Na John Bukuku, Dar es Salaam
Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imejipambanua kama chombo makini cha kuzalisha maarifa na ushahidi wa kisayansi unaotumika katika kufanya maamuzi ya kisera kuhusu elimu nchini. Kupitia tafiti mbalimbali bunifu, TET imeendelea kuibuka kama daraja muhimu linalounganisha elimu ya kitaalamu na uhalisia wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia Tanzania.
Akizungumza katika semina ya wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 13, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, amesema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto halisi zinazoikumba sekta ya elimu, hususan maeneo ya vijijini, kwa kutumia tafiti zenye ushahidi wa kisayansi.
Miongoni mwa tafiti zenye matokeo halisi ni ile ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambayo iliangazia teknolojia rafiki kwa walimu walioko maeneo ya vijijini. Utafiti huo ulifanyika kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Aga Khan University, Aga Khan Foundation na EdTech Hub, na uligharimu Shilingi milioni 850.
“Matokeo ya utafiti huu yameanza kusaidia kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya teknolojia za TEHAMA zinazofaa zaidi kwa mazingira ya vijijini ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi,” alisema Dkt. Komba.
Katika mwaka wa fedha 2021/2022, TET ilitekeleza utafiti mwingine kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Western Norway of Applied Sciences, uliolenga kutambua changamoto za uoni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi. Utafiti huo, uliojulikana kama Kuona ni Kujifunza, uligharimu Sh. milioni 950 na kuibua hitaji la kuandaliwa kwa moduli maalum kwa ajili ya mafunzo kazini kwa walimu.
“Hii itawasaidia walimu kuwabaini na kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto za kuona katika hatua za awali kabisa za ujifunzaji,” alifafanua.
Katika hatua ya kimkakati, TET inatekeleza utafiti wa miaka mitano wa kimataifa kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya Georgetown, Delaware na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia mpango wa What Works Hub for Global Education.
Kupitia mpango huo, TET imeanzisha kituo cha tafiti bunifu kijulikanacho kama TIE-Ed-Lab, ambacho kimejikita kwenye uzalishaji wa maarifa na njia mpya za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia ushahidi. Utafiti huo utagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 7 kwa kipindi chote.
Kwa mujibu wa Dkt. Komba, hadi kufikia mwaka 2025, TET imeingia mikataba 35 ya ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi, nyingi zikiwa kwenye nyanja za matumizi ya akili mnemba (AI) na utayarishaji wa maudhui ya kidijitali.
“Huu ni ushahidi kuwa sekta ya elimu nchini inafaidika moja kwa moja na tafiti zetu, hususan kwa kubuni suluhisho la changamoto zinazowakabili walimu na wanafunzi katika mazingira halisi ya shule zetu,” alisema.
Kwa miaka 50 sasa, TET imethibitisha kuwa utafiti si kazi ya kimaandishi tu, bali ni nyenzo ya kimkakati inayobadili maisha, kuongeza maarifa, na kuhakikisha mfumo wa elimu wa Tanzania unakuwa na msingi imara wa kitaalamu na ushahidi wa kisayansi.