Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayemaliza muda wake, Dkt. Akinwumi Adesina amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 4 aliyoifanya nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 hadi 15 Juni 2025.
Dkt. Adesina aliondoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kusindikizwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo.
Ziara ya Dkt. Adesina nchini imetokana na mwaliko kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa madhumuni ya kutembelea miradi ambayo benki hiyo imetoa fedha ya kuigharamia.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na barabara ya mzunguko ya Dodoma ambayo kwa pamoja Rais Samia na Dkt. Adesina waliitembelea jijini Dodoma Juni 14, 2025.
Dkt. Adesina ni Rais wa 8 wa AfDB na katika uongozi wake amefanya mageuzi makubwa katika benki hiyo na kuifanya kuwa chombo imara, chenye mtaji wa kutosha na utaalamu wa kuchagiza mageuzi ya kiuchumi barani Afrika hususan katika sekta za miundombinu, kilimo, afya, nishati, mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya kifedha.
Kutokana na mchango mkubwa alioutoa barani Afrika, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kilimtunikia Shahada ya Heshima ya Falsafa katika Sayansi katika mahafali ya 55, duru ya kwanza yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Juni 13, 2025.