Serengeti
Shirika la Grumeti Fund limefanikiwa kuwezesha vijiji 21 vinavyozunguka Hifadhi na Mapori ya Akiba ya Grumeti wilayani Serengeti, mkoani Mara, kuachana na vitendo vya uwindaji haramu na uharibifu wa mazingira kwa kuwapatia wananchi njia mbadala ya kiuchumi kupitia utengenezaji wa batiki.
Afisa Mradi wa Ustawishaji Biashara Vijijini kutoka Grumeti Fund, Nelson Petro, amesema kuwa utengenezaji wa batiki umeonekana kuwa mbinu bora ya kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kujipatia kipato halali na endelevu badala ya kutegemea shughuli haramu kama uwindaji na uchomaji wa mkaa.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wanafunzi wa utengenezaji wa batiki yaliyofanyika katika Kijiji cha Parknyigoti, Petro alisema kuwa programu hiyo inalenga kujenga jamii endelevu kiuchumi na inayoshiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi.
“Kwa muda mrefu wananchi waliokuwa wakizunguka hifadhi walitegemea uwindaji na uchomaji wa mkaa kama njia kuu ya kujikimu kimaisha. Sasa tumeanzisha mradi huu wa batiki ili kuwapatia fursa mpya ya biashara ambayo ni rafiki kwa mazingira,” alisema Petro.
Aliongeza kuwa Grumeti Fund inaamini katika kuibua na kukuza vipaji vya wananchi hususan vijana na wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa mazingira na kuendeleza uhifadhi kupitia uchumi mbadala.
Mpango huo wa batiki ni sehemu ya juhudi za shirika hilo za kuhamasisha uhifadhi shirikishi kwa k
uhakikisha kuwa jamii zinazozunguka hifadhi zinanufaika moja kwa moja na uwepo wa rasilimali za asili.