……………..
Na Sixmund Begashe – Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii imepongezwa kwa kazi kubwa ya Uhifadhi wa Maliasili nchini na kukuza Utalii hali inayochangia kwa kiasi kukubwa kwenye pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mbunge), Jijini Dodoma, alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali Park.
Mhe. Simbachawene amesema kazi inayofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja ili urithi adhimu wa Maliasili nchini uendele kunufaisha kizazi kilichopo na kinachokuja.
Aidha licha ya kuipongeza Wizara hiyo kwa ushiriki katika maonesho hayo makubwa, Mhe. Simbachawene, amewasisitiza watumishi hao kuhakikisha wanaitumia vyema wiki ya maonesho hayo katika kuwahudumia wananchi watakaotembelea banda hilo.
Naye Mwenyekiti wa Maonesho ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nassoro Wawa, ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda hilo ili kujipatia huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara kupitia Idara na Taasisi zake katika kipindi chote cha maonesho hayo.