Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Upendo Matotola akizungumza wakati wa Kikao cha Wadau wa Sekta ya Milki kilichofanyika jijini Mwanza tarehe 17 Juni 2025. Kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Wilson Luge.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Wilson Luge akizungumza kwenye kikao cha wadau wa sekta ya milki kilichofanyika jijini Mwanza tarehe 17 Juni 2025.
Washiriki wakiwa katika kikao cha wadau wa sekta ya milki kilichofanyika jijini Mwanza tarehe 17 Juni 2025.
Nuru Kimbe Afisa kutoka Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwasilisha mada wakati wa kikao cha wadau wa milki jijini Mwanza tarehe 17 Juni 2025. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
…………
Wadau wa sekta ya milki nchini wametakiwa kuendelea kuwa na umoja ili kuhakikisha sekta ya milki inakuwa.
Hayo yameelezwa tarehe 17 Juni 2025 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Upendo Matotola wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya milki kilichofanyika mkoani Mwanza.
Kikao hicho ni muendelezo wa mijadala mbalimbali kati ya kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau wa Sekta ya Milki kwa lengo la kujenga ufahamu na kupata maoni kuhusiana na sekta ya milki nchini.
Tayari kitengo hicho kimefanya vikao vya mijadala katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha na Dodoma.
” Ni lazima tuwe wamoja na kuhakikisha sekta yetu ya milki inakuwa sambamba na kuwa na sura nzuri” amesema
Kwa mujibu wa Dkt Matotola, wananchi wakishaiamini sekta ya milki kazi itakuwa rahisi ikiwemo upatikanaji kazi nyingi kwa kuwa wananchi hawatakuwa na haja ya kuhangaika kutokana na uwepo wa watu wanaowaamini.
” Kwa sababu mtu hana sababu ya kuhangaika kutafuta nyumba au kiwanja maana kuna watu wanawaamini na serikali inawaamini pia hivyo tunaweza kufanya kazi vizuri”. Ameeleza
Mkurugenzi huyo wa Kitengo cha Milki ameweka wazi kuwa, kikubwa serikali inachotaka ni kujua kutoka kwa wadau zile changamoto wanazozipata katika uendeshaji na kile wanachotegemea kutoka kwa serikali ili kutengeneza mazingira bora ya kuwafanya wadau kufanya kazi vizuri.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Wilson Luge amesema, serikali imeona ipo haja ya kuzungumza na wadau wa sekta ya milki ili kuwa na uelewa wa pamoja.
” Tutembee pamoja, sisi tuna malengo ya kufikia hatua fulani lakini na ninyi mna malengo fulani hivyo malengo yetu yaende sambamba na malengo yenu” amesema Luge.
Katika kikao hicho cha wadau wa sekta ya milki washiriki walipata uelewa wa majukumu ya kitengo cha milki, mfumo wa usajili na faida zake kwa mawakala, utakatishaji fedha katika sekta na wajibu wa mawakala katika kupambana na utakatishaji pamoja na mwongozo wa usajili wa mawakala.