Na John Buluku Pwani, Juni 19, 2025,
Wakati Kampuni ya Bakhresa Group (SSB) ikiwa inaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, waandishi wa habari wametembelea kiwanda cha Bakhresa Food Products Ltd (BFPL) kilichopo Mwandege, mkoani Pwani, kwa lengo la kujionea na kujifunza namna kinavyozalisha vinywaji baridi kuanzia hatua ya uchakataji wa matunda.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo, Afisa Ubora wa BFPL, Charles Hayola, alisema kampuni imefanya upanuzi mkubwa kwa kufunga mitambo mipya ya kisasa ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutoka kwa wateja.
“Awali tulikuwa tukizalisha kati ya katoni 150,000 hadi 200,000 kwa siku, lakini baada ya kufunga mitambo mipya, sasa tuna uwezo wa kuzalisha kati ya katoni 250,000 hadi 300,000 kwa siku,” alisema Hayola.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo inazingatia viwango vya ubora kuanzia upatikanaji wa malighafi hadi hatua ya mwisho ya uzalishaji, kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na viwango vya kimataifa (ISO).
Kwa upande wake, Meneja Ubora wa Kitengo cha Matunda, Bi. Bakila Elson, alisema kampuni imekuwa ikitoa elimu kwa wakulima kuhusu aina na ubora wa malighafi zinazohitajika, huku zikichunguzwa kwa kina ili kuhakikisha bidhaa bora na salama zinapatikana.
Naye Meneja wa Kitengo cha Upakiaji na Usafirishaji, Bw. Simon Kalando, alisema BFPL inasafirisha bidhaa zake ndani na nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.
“Tunasafirisha bidhaa zetu Afrika Mashariki na Kati, lakini pia nje ya bara la Afrika kama vile Yemen na Oman. Jana tu tumetuma bidhaa Yemen na wiki iliyopita tulipeleka Oman,” alisema Kalando.
Kampuni ya Bakhresa Food Products Ltd ni miongoni mwa waajiri wakubwa nchini, ikiwa imeajiri zaidi ya watu 1,000 moja kwa moja. Pia, imekuwa ikiongeza thamani ya mazao ya matunda ya wakulima wa ndani, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.