Afisa Tawala na Rasilimali watu NBAA, Gloria Kaaya akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno kuhusu mikakati ya kuanzisha kanzi data (database) ya wanafunzi wanaosomea masomo ya uhasibu katika vyuo mbalimbali nchini kwa wakuu wa Idara za Fedha na Uhasibu vyuoni.
BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeweka mikakati ya kuanzisha kanzi data (database) ya wanafunzi wanaosomea masomo ya uhasibu katika vyuo mbalimbali nchini, ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo yao kitaaluma na kuwasaidia katika maandalizi ya mitihani ya Bodi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, Afisa Tawala na Rasilimali Watu wa NBAA, Bi. Gloria Kaaya, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taaluma ya uhasibu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata taarifa sahihi kwa wakati kuhusu masuala ya kitaaluma.
“Tumeanzisha mpango huu ili kuwatambua na kuwafuatilia wanafunzi wote wanaosomea uhasibu vyuoni. Kupitia “database” hii, tutawawezesha kupata taarifa muhimu kuhusu taratibu za mitihani, masharti ya kupata misamaha “exemptions”, na muda sahihi wa kuanza mitihani ya kitaaluma baada ya kuhitimu,” alisema Bi. Kaaya.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikosa fursa ya kufanya mitihani ya Bodi kwa wakati kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi, au kuchelewa kujiandikisha ndani ya muda unaotakiwa, hasa pale inapozidi miaka mitano tangu kumaliza masomo yao.
Kwa mujibu wa NBAA, “database” hiyo pia itarahisisha mawasiliano kati ya Bodi, vyuo vya elimu ya juu na wanafunzi wenyewe, hivyo kuongeza uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma nchini.
“Tunataka wanafunzi wote waelewe fursa walizonazo na wajue hatua wanazopaswa kuchukua ili kufikia malengo yao ya kitaaluma. Mfumo huu utasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu waliothibitishwa, ambao ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisisitiza.
NBAA imetoa wito kwa taasisi za elimu ya juu kushirikiana na Bodi hiyo katika utekelezaji wa mpango huu kwa kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinasajiliwa kwa usahihi, huku ikiwataka wanafunzi kufuatilia matangazo rasmi ya Bodi hiyo kupitia tovuti na mitandao yake ya kijamii.
Baadhi ya wakuu wa Idara za Fedha na Uhasibu vyuoni pamoja na watumishi wa NBAA wakifuatilia mada
Picha ya pamoja