Na. Edmund Salaho/Katavi
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji jana tarehe 22 Juni, 2025 alifanya ziara ya kikazi na kufanya kikao na Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Katavi iliyopo mkoani Katavi.
Kamishna Kuji, alisisitiza kuwa kila mtumishi ana haki ya kujiendeleza kielimu, haki ya kupata matibabu bora, kupata likizo pamoja na haki ya kupandishwa cheo pale anapotimiza vigezo vyote vya kiutumishi na haki ya kuthaminiwa kutokana na kazi anayoifanya.
Katika kikao hicho Kamishna Kuji alibainisha kuwa kila mtumishi ana haki husika ambapo pia Mwajiri anayo matarajio ya kuona uwajibikaji madhubuti kutoka kwao.
“Uhifadhi na Utalii unahitaji kuwa na wataalamu wa kila nyanja, na Jeshi lenye wasomi wengi ndio lenye ufanisi mkubwa katika kutekeleza majukumu yake, hivyo ni lazima Maafisa na Askari Uhifadhi wapate “exposure” ndani na nje ya nchi kwani ziara za aina hiyo husaidia kuongeza uelewa wa mifumo ya Ikolojia, ufuatiliaji wa wanyamapori, utambuzi wa viashiria vya uhalifu katika hifadhi, pamoja na matumizi ya teknolojia mpya kwa ufanisi. Nitoe rai kwa kila Afisa na Askari Uhifadhi kujiendeleza kielimu kwani Shirika limeweka mazingira bora ya kujiendeleza”, alisema Kamishna Kuji.
Awali, akimkaribisha Kamishna wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Katavi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kusini, Godwell Meng’ataki alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha Uhifadhi na Utalii hususani kwa hifadhi zilizopo Kusini, kwani zimekuwa zikipokea idadi kubwa ya watalii kwa sasa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“Tumeshuhudia idadi kubwa ya watalii, kipekee shukrani zetu zimfikie Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake kwani kupitia Filamu yake maarufu ya Tanzania: The Royal Tour” na ile ya “Amazing Tanzania” Hifadhi za Taifa zilizopo Kusini tumeanza kuona matunda yake kwa kuongeza idadi ya watalii na wawekezaji wanaokuja kuwekeza kwenye maeneo haya”. alisema Kamishna Meng’ataki
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Emilian Kihwele ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Katavi
ameipongeza Bodi ya Wadhamini TANAPA pamoja na Menejimeti ya Shirika kwa namna ambavyo imekuwa ikiwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kuongeza kuwa kwa mwaka fedha ujao wa 2025/2026, Hifadhi ya Taifa Katavi imejipanga vilivyo katika kuhifadhi na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo pamoja mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Maafisa na Askari Uhifadhi wa hifadhi hiyo wamepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali na Shirika kwa namna Viongozi wanavyowafikia katika maeneo yao ya kazi na kuwasikiliza na kupanga kwa pamoja mikakati ya kupeleka mbele maendeleo ya taasisi katika kuimarisha uhifadhi na kuongeza mapato kupitia shughuli za utalii.
“Nikupongeze Afande Kamishna Kuji, licha ya majukumu uliyonayo unatoka na kuja kuzungumza na askari, tumekuona ukizungumza na askari katika hifadhi mbalimbali za Taifa na sasa umefika hapa Katavi. Ukaribu huu kwetu unatia hamasa na kuongeza morali zaidi ya kuchapa kazi” alisema Askari Uhifadhi Daraja la Kwanza Erasto Majabe (Hifadhi ya Taifa Katavi).
Serikali kupitia TANAPA inaendeleza jitihada za kuboresha miundombinu ya utalii katika maeneo ya nyanda za juu kusini ili kuwezesha watalii wengi kupata fursa ya kutembelea maeneo yaliyohifadhiwa katika ukanda huo na kupunguza uhitaji wa watalii kutalii katika maeneo ya kaskazini pekee.