Jamii imeaswa kujenga utamaduni wa kua na moyo wa kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji haswa Watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kutokana na wazazi wengi kushindwa kumudu gharama za matibabu ya ugonjwa huo.
Wito huo umetolewa na Grace Mollel ambaye ni mmoja ya mzazi wa mtoto mwenye changamoto ya vichwa vikubwa aliyefanyiwa upasuaji katika Taasisi ya mifupa MOI kupitia ufadhili wa taasisi ya LALJI FOUNDATION.
Akizungumza baada ya upasuaji wa mtoto wake ameishukuru taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa msaada huo kwani hakua na uwezo wa kumudu gharama za matibabu hivyo kupitia msaada wao umefanikisha kurejesha tabasamu kwani mtoto wake amefanyiwa upasuaj na anaendelea na matibabu.
Aidha ametoa wito kwa watu wenye uwezo kujitoa kusaidia watu wenye uhitaji maalum haswa Watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kwani wazazi wengi wenye Watoto wenye changamoto hiyo hawana uwezo wa kumudu gharama za upasuaji.
Pia amewashauri wazazi wa Watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa kuwapeleka hospitali mapema ili wapatiwe huduma za matibabu kwani kuwafungia ndani kunaweza kuleta athari kubwa zaidi .
Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya uti wa mgongo na mishipa ya fahamu Hospitali ya MOI Hamisi Shabani amesema tatizo la Vichwa kikubwa na mgongo wazi ni kubwa kiasi lakini kwa sasa limeanza kuonekana kwa wingi kutokana na uelewa wa jamii kuhusu tatizo hilo.
” Tunawashukuru watanzania ambao wameweza kutoa elimu mbalimbali kuhusu kuzuia unyanyapaa wa Watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi na idadi wa wazazi kuwapeleka Watoto hospitali imekua inaridhisha kutokana na uelewa wa jamii kuhusu tatizo hilo.
Amesema kwa wastani nchi ya Tanzania inazalisha takribani Watoto 4000 wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa mwaka kwa ikiwa ni kwa mujibu wa makisio ya sensa ya mwaka 2022 ambayo inafafanua kuwa takribani Watoto elfkumi wanaozaliwa Watoto watatu wanazaliwa na changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Amesisitiza kuwa tatizo la vichwa vikubwa linazuilika kwa mama mjamzito endapo timu ya wataalamu itajiridhisha kuwa mama huyo hana tatizo la upungufu wa madini ya folic na akigundulika ana changamoto ya upungufu wa madini hayo basi atapewa vidonge kwaajili ya kuongeza madini hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanasaidia kuzuia tatizo hilo.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa taasisi ya LALJI FOUNDATION Mohamed Damji amesema kwa kushrikiana na MOI wametoa msaada huo ili kusaidia Watoto hao ambao wazazi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za upasuaji ikiwa ni sehemu ya majukumu ya taasisi hiyo kusaidia watu wenye uhitaji.
Aidha ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia Watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa kwani tatizo bado lipo na wenye uhitaji na msaada huo ni wengi na hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Ameongeza kuwa taasisi ya LALJI FOUNDATION itaendelea kushirikiana na MOI kufadhili upasuaji wa Watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na kusisitiza kuwa zoezi hilo litakua endelevu kwa lengo la kuwafikia Watoto wengi zaidi.