Mkurugenzi Mtendaji wa Makumbusho ya Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi, Ol-aiguenani Meshack Ndaskoi akitoa maelezo kwa wanafunzi hao kuhusu historia mbalimbali.

Wanafunzi hao wakitembelea makumbusho hiyo iliyopo Moshono jijini Arusha.


Wanafunzi hao wakipanda miti ishara ya Kumbukumbu yao kutembelea makumbusho hiyo jijini Arusha .
………………..
Happy Lazaro, Arusha
WANAFUNZI wa Skauti zaidi ya 100 kutoka Shule za Tusiime zilizoko Tabata, Ilala Mkoani Dar es Salaam wamefanya ziara ya kimafunzo ya kutembelea Mkoa wa Arusha ambapo mojawapo ya maeneo waliyotembelea ni Makumbusho ya Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi iliyoko Moshono Jiji la Arusha.
Makumbusho hii binafsi ni ya kipekee katika Mkoa wa Arusha inayoonesha historia ya Jiji la Arusha tangu mwishoni mwa karne ya 16 kabla ya ujio wa wakoloni, wakati wa ukoloni na baada ya Uhuru pamoja na utamaduni wa jamii ya Wamaasai na Wameru.
Sambamba na maonesho haya ipo bustani ambayo ni sehemu ya Makumbusho inayotunza miti na mimea ya asili na mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kiongozi wa ziara hiyo Mwl. Goodluck Karashani amesema, Shule za Tusiime chini ya “Tanzania Scout Association” (TSA) wamekuwa na utaratibu wa kufanya ziara ya kimafunzo kwa wanafunzi wao kwa kutembelea maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi hususan wakati wa likizo ndefu.
“Na uzoefu umeonyesha kwamba utaratibu huu umekuwa na manufaa makubwa sana kwa wanafunzi kwani kupitia ziara hizo wameweza kupanua na kuimarisha uelewa, maarifa na stadi zao katika masuala mbalimbali wanayojifunza nje ya darasa.”amesema .
Kwa mantiki hii lengo kuu la kutembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi ni kuwawezesha wanafunzi kujifunza urithi wetu wa kihistoria na kiutamaduni hususan historia ya Arusha na utamaduni wa jamii maarufu ya Kimaasai ambao Makumbusho hii imejikita.
“Nikiri kwamba wanafunzi n ahata sisi waalimu tulioambatana nao tumeweza kujifunza mambo mengi kuhusu historia na utamaduni wa Jamii ya Wamaasai kupitia vifaa na vyombo halisi kutoka katika jamii hii. “amesema .
“Vilevile tumejifunza kuhusu mchango mkubwa uliotolewa na jamii ya Wamaasai katika kupinga ukoloni wakiongozwa na kiongozi wao Mkuu, Chifu Ndaskoi jambo ambalo halifahamiki vizuri na watu walio wengi kwa kuwa haijaandikwa vya kutosha kwenye historia ya nchi yetu. “amesema
Aidha ametoa wito kwa jamii na wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya elimu ya kati na vya Juu kutembelea Makumbusho hii ambayo imesheheni utajiri mkubwa wa urithi wetu kihistoria, kitamaduni na kishujaa ili kuweza kujionea na kujifunza zaidi.
“Wanafunzi kwa upande wao walieleza, kwamba tumejifunza mambo mengi ambayo hatukuyafahamu kabla ya hapo kupitia vifaa na vyombo halisi vilivyotumiwa na watu wa zamani. Pia tumejifunza historia ya Jiji la Arusha tangu karne ya 16 hadi sasa na mila na desturi nzuri za jamii Wamaasai na kutambua upotoshaji uliopo kuhusu baadhi ya mila za desturi hizo,Mambo haya yote yatatusadia katika masomo yetu tukirudi shuleni.”amesema .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Makumbusho ya Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi, Ol-aiguenani Meshack Ndaskoi, ameupongeza uongozi wa Shule za Tusiime kwa kutambua umuhimu wa kuwaleta wanafunzi katika Makumbusho hiyo na kusema ni ukweli usiopingika kwamba Makumbusho ni taasisi muhimu katika jamii ikizingatiwa kwamba kimsingi zipo kwa ajili ya kutoa elimu, kutafiti, mawasiliano na kutoa burudani.
Aidha amesema kuwa ,Makumbusho ya Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi imeanzishwa kwa nia ya kukusanya, kuhifadhi, na kukuza hazina ya urithi wetu wa kihistoria na kiutamaduni kwa ajili manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha imepewa jina la Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi kama njia ya kumuenzi kutokana na mchango wake mkubwa ambao kwa bahati mbaya haufahamiki na watu walio wengi.
” Michango aliyotoa ni pamoja na kuasisi jiji la Arusha, kuongoza mambabano dhidi ya ukoloni, kuwasaidia Wamisionari wa kwanza kuanzisha na kuendeleza dini, kulinda na kuhifadhi utamaduni na mila, kuhamasisha na kuhimiza wazazi kupeleka watoto wao wa kike shule sawa na wa kiume na kulinda na kutunza mazingira.”amesema .
Aidha ametoa wito kwa watafiti, wanazuoni, watalii wa ndani na nje na jamii kwa ujumla kuitambua na kuitumia kikamilifu ili iweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake maana inatuwezesha kujua wapi tulikotoka, mahali tulipo na tunakokwenda,jambo ambalo ni la msingi katika jamii kwani huleta shauku ya kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa njia endelevu katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kisanyansi na kiteknologia.
Aidha katika ziara hiyo wanafunzi walipata fursa adhimu ya kushiriki tendo la kihistoria la kupanda miti ya asili katika Bustani ya kutunza miti na mimea ya asili katika Chief Ndaskoi Botanical Garden ambayo ni mwanachama wa Botanical Garden Conservation International (BGCI 5442). Miti waliyootesha hujulikana kwa Kimaasai kama Ol-oirien (Olea europaea) ambayo ni mojawapo kati ya miti takatifu kwa jamii ya Wamaasai.