Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara akipokea zawadi kutoka kwa Lwaga Mwambande Mkuu wa Mawasiliano Bodi ya Bima ya Amana DIB wakati alipotembelea katika banda Hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Bima ya Amana Bw. Isack Kihwili akikabidhi zawadi kwa Meneja wa Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania wakati aliyetembelea katika banda Hilo ili kuona shughuli zao katika maonesho hayo.
,…..
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imeshiriki katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulinzi wa amana zao katika taasisi za fedha zilizosajiliwa kisheria.
Katika kuonesha umuhimu wa taasisi hiyo katika sekta ya fedha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, alitembelea banda la DIB na kupokea maelezo kutoka kwa Bw. Silvani Makore kuhusu shughuli na majukumu ya Bodi hiyo. Prof. Kahyarara alipongeza juhudi za DIB katika kuchangia utulivu wa sekta ya fedha na kuwataka wananchi kuendelea kutumia huduma za kibenki kwa kujiamini, wakitambua kuwa amana zao zinalindwa kupitia mfumo wa bima ya amana.
Kwa mujibu wa maofisa wa DIB waliopo katika banda hilo, wananchi wamekuwa wakipatiwa elimu ya kina kuhusu huduma hiyo ya ulinzi wa fedha zao, namna mfumo unavyofanya kazi, na kiasi cha fidia kinachotolewa kwa mteja endapo benki itafungwa rasmi na Benki Kuu ya Tanzania. Imeelezwa kuwa fidia ya hadi shilingi milioni 1.5 hutolewa kwa kila mteja kwa haraka ndani ya siku chache baada ya taasisi husika kufungwa.
Aidha, kupitia banda hilo, DIB imeendelea kuhamasisha wananchi kuhifadhi fedha zao katika taasisi rasmi za kifedha zilizosajiliwa, kwa kuwa ndizo pekee zinazotambuliwa na kulindwa na mfumo huo wa bima ya amana. Wananchi walioshiriki wameonesha kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema itawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Maonesho haya yamekuwa jukwaa muhimu kwa DIB kufikisha ujumbe wake kwa jamii kuhusu ulinzi wa fedha, huku Bodi hiyo ikitumia fursa hiyo kuongeza uelewa wa umma kuhusu wajibu wake na namna inavyosaidia kuimarisha uaminifu na uthabiti wa sekta ya fedha nchini.