Na John Bukuku, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 tarehe 17 Julai 2025, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Uzinduzi huo utafanyika wakati wa Mkutano wa Tatu wa Taifa wa Dira, na unatajwa kuwa ni tukio kubwa la kihistoria, likiwa ni mara ya pili kwa Tanzania kuandaa dira ya muda mrefu ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza na Jukwaa la Wahariri (TEF) katika mkutano uliofanyika Julai 2025 kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kuwa mchakato wa maandalizi ya Dira 2050 umehusisha ushirikiano mpana wa kitaifa na kimataifa, huku maoni ya Watanzania kutoka makundi mbalimbali yakichangia msingi wa dira hiyo.
“Dira hii siyo ya chama chochote, ni dira ya Watanzania wote. Vyama vya siasa vinaelewa kwamba ilani zao zinapaswa kuakisi dira hii. Hatutarajii kuona chama chochote kikitunga ilani inayokwenda kinyume na Dira ya Taifa,” alisema Profesa Mkumbo.
Alifafanua kuwa Dira 2050 imejengwa kutokana na maoni ya wananchi waliokusanywa kupitia vikao vya wadau kutoka sekta zote ikiwemo vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, wanataaluma, waandishi wa habari na makundi ya kijamii, ili kuleta maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa taifa.
Katika kufanikisha uandishi wa dira hiyo, Prof. Mkumbo alisema timu ya wataalamu ilijifunza kutoka nchi mbalimbali kama Morocco, Mauritius, Kenya, Afrika Kusini, China, India, Indonesia, Singapore, Vietnam na Korea Kusini – nchi ambazo ziliwahi kuwa katika hatua za maendeleo zinazofanana na Tanzania, lakini kwa sasa zimepiga hatua kubwa kimaendeleo.
“Tumewaangalia Vietnam na Singapore walivyoongeza thamani ya bidhaa zao, na namna walivyotumia dira madhubuti kusukuma maendeleo. Haya ni mafunzo muhimu kwetu,” aliongeza.
Baada ya hatua ya ukusanyaji wa data, uandishi, uhariri na uchambuzi wa kitaalamu, rasimu ya kwanza ya dira iliwasilishwa kwa wananchi kutoa maoni yao. Hatua iliyofuata ilikuwa ni mchakato wa makabidhiano kwa makundi mbalimbali ya kijamii, mashirika ya ndani na ya kimataifa yanayoshirikiana na Tanzania, ili kuhakikisha mipango yao ya misaada, mikopo na miradi inaendana na maudhui ya dira.
Rasimu ya pili ya dira iliwasilishwa kwa Waziri Mkuu kama maoni yaliyopendekezwa na Watanzania, kabla ya kukabidhiwa kwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji ili kuingizwa katika mchakato wa maamuzi wa serikali kwa kushirikisha makatibu wakuu.
Hatimaye, tarehe 22 Juni 2025, Baraza la Mawaziri liliidhinisha rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kisha kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kuridhiwa.
Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo, Dira hii itaongoza maendeleo ya nchi kwa zaidi ya miongo miwili ijayo, chini ya usimamizi wa marais watakaoingia madarakani hadi mwaka 2050.
“Lengo letu ni kuhakikisha mjadala wa kisiasa unajikita katika namna ya kufika kwenye malengo ya maendeleo, na si kuhusu kwenda wapi – kwa sababu tumeshaamua, kama taifa, tunataka kwenda wapi,” alisisitiza.