Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS), Dkt. Fidelice M.S. Mafumiko akiwasilisha mada kwa wahariri wa vyombo vya habari katika kikaokazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika Kwenye hoteli ya King Jada jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano Ofisi ya Masajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri akizungumxa katika kimao hicho.
………..
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS), Dkt. Fidelice M.S. Mafumiko amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya uwekezaji mkubwa katika mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara nchini.
Dkt. Mafumiko ameyasema hayo Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha mada mbele ya wahariri na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika katika Hoteli ya King Jada, Morocco Square.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo umewezesha ongezeko la thamani ya mitambo kutoka Shilingi Bilioni 13.6 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Shilingi Bilioni 17.8 mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.6. Kiasi hicho kimetumika kununua mitambo mikubwa 16 na midogo 274, hatua iliyosaidia kuboresha ufanisi wa uchunguzi wa kimaabara kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na MMS, Dkt. Mafumiko alisema kuwa mamlaka imefanikiwa kutoa huduma za uchunguzi wa kimaabara zinazokubalika kitaifa na kimataifa kwa kutekeleza mifumo ya ubora na umahiri yenye viwango vya kimataifa kama ISO 9001:2015 na ISO 17025:2027.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, MMS imefanikiwa kupata ithibati ya mfumo wa umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO 17025:2027) katika maabara sita ambazo ni: Maabara ya Vinasaba vya Binadamu, Mikrobiolojia, Sayansi Jinai, Toksikolojia, Mazingira, Maabara ya Chakula na Kanda ya Ziwa – Mwanza.
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa kemikali, Dkt. Mafumiko alisema Mamlaka inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Na. 3 ya mwaka 2003. Sheria hiyo inalenga kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari za kemikali.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita ni pamoja na:
Usajili wa Wadau: Idadi ya wadau waliosajiliwa imeongezeka kutoka 2,125 mwaka 2021 hadi kufikia 3,835 Juni 2025, ongezeko la asilimia 81.
Ukaguzi wa Maghala: MMS imekagua maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali, ikiwa ni asilimia 119 ya lengo la ukaguzi wa maghala 7,160.
Vibali vya Kuingiza/Kusafirisha Kemikali: Vibali vya kuingiza kemikali vimeongezeka kutoka 40,270 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 67,200 mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 40.
MMS pia imechangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini, hasa zile zinazotumika katika sekta ya madini. Dkt. Mafumiko alieleza kuwa matumizi ya kemikali muhimu yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka minne:
Ammonium Nitrate: Tani 135,445 mwaka 2021/2022 hadi Tani 461,777.42 mwaka 2025 (ongezeko la asilimia 241).
Salfa: Tani 396,982 mwaka 2021/2022 hadi Tani 1,867,104.72 mwaka 2025 (ongezeko la asilimia 370.32).
Sodium Cyanide: Tani 41,461 mwaka 2021/2022 hadi Tani 63,103.4 mwaka 2025 (ongezeko la asilimia 52.20).
Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya shehena ya Ammonium Nitrate huingia kupitia Bandari ya Tanga, jambo linaloonyesha mafanikio ya uwekezaji wa serikali katika miundombinu ya bandari hiyo.
Dkt. Mafumiko amehitimisha kwa kusema kuwa mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za kisayansi, kudhibiti kemikali hatarishi na kuhakikisha usalama wa wananchi na mazingira.