Ubalozi wa Tanzania na Serikali ya Comoro zimekubaliana kuendeleza mazungumzo ya kuanzisha ufundishwaji wa Kiswahili mashuleni kufuatia ahadi ya Rais Samia ya kutoa walimu na vifaa kwa shule za nchi hiyo.
Maelezo hayo yametolewa na Balozi wa Tanzania,Saidi Yakubu na Waziri wa Elimu wa Comoro,Bacar Mvoulana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili nchini Comoro yaliyofanyika katika mji wa Ntsaoueni na kuhudhuriwa na Gavana wa Kisiwa hicho,Mawaziri na Balozi Mdogo wa Afrika Kusini,Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa,Asasi za Kiraia na Wananchi wa miji 11 inayozungumza Kiswahili katika Kisiwa cha Ngazidja.
Akizungumza katika hafla hiyo Balozi Yakubu alirejea kauli ya Rais Samia aliyoitoa nchini humo wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru kuwa Tanzania inaishauri Comoro kuangalia uwezekano wa kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zake rasmi na Serikali yake itakuwa tayari kutoa walimu na vifaa vya kufundishia ili kufanikisha azma hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Mvoulana alieleza faraja ya Serikali ya Comoro kwa ahadi hiyo na Wizara yake itajipanga kwa tathmini kamili ya mahitaji huku mjadala wa ufundishaji ukiendelea.
Sherehe hizo za Kiswahili zilipambwa na Burudani ya Taarab ya Mzee Yusuf kutoka Tanzania,kikundi cha Taarab Ayn cha Comoro,mchezo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu,ngoma ya Lelemama toka kundi la Salama Mapesa na mada mbali mbali kuhusu nafasi na fursa za Kiswahili nchini Comoro.