Dodoma, Julai 2025
Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum imeeleza kuwa mafanikio makubwa ya kampeni ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni yametokana kwa kiwango kikubwa na utekelezaji wa elimu mashuleni kwa wanafunzi na walimu kote nchini.
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha Kamati ya Taifa ya Kumlinda Mtoto Mtandaoni (COP), ambapo ripoti ya tathmini ya kampeni hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Aprili 2025 inawasilishwa kwa wadau.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kampeni imefanikiwa kuwafikia jumla ya wanafunzi 1,821,593 wa shule za msingi na sekondari kupitia warsha, midahalo na maonyesho ya elimu ya usalama wa mtoto katika mitandao. Vilevile, walimu 3,909 kutoka shule mbalimbali walipatiwa mafunzo ya namna ya kutambua na kukabiliana na changamoto za usalama wa kidijitali miongoni mwa wanafunzi.
Katika utekelezaji huo, shule 779 za msingi na 209 za sekondari zilitembelewa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara. Timu ya kampeni, kwa kushirikiana na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii na Elimu kutoka halmashauri husika, ilitoa elimu ya ana kwa ana kwa wanafunzi ikihusisha matumizi salama ya intaneti, madhara ya kushiriki mazungumzo na watu wasiojulikana mitandaoni, na umuhimu wa kuripoti vitisho au manyanyaso kwa watu wazima wanaoaminika.
“Watoto wengi walijifunza dhana mpya kama nyayo za kidijitali, kutotuma picha binafsi, na namna ya kujilinda dhidi ya watu wanaojifanya marafiki kwenye mitandao. Hili limeongeza ujasiri na uelewa kwa kiwango kikubwa,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Aidha, kampeni hiyo imesababisha kuanzishwa kwa madawati ya usalama wa mtoto mtandaoni katika shule nyingi, ambapo walimu wa malezi na unasihi wamepewa jukumu la kuratibu utoaji wa elimu endelevu na kuwa sehemu ya kwanza ya kupokea taarifa za vitendo vya ukatili wa mtandaoni.
Katika kikao hicho, ilielezwa kuwa baadhi ya shule zimeshaanzisha pia kamati ndogo za usalama wa mitandao zinazoongozwa na wanafunzi walioelimishwa, kwa lengo la kusaidia wenzao kuelewa namna ya kutumia mitandao kwa usalama.
Kampeni pia iliwahusisha wazazi na walezi kupitia vikundi vya malezi chanya, ambapo zaidi ya wazazi 35,000 walipatiwa elimu hiyo. Vikundi hivyo vimekuwa chachu ya kueneza ujumbe wa ulinzi wa mtoto mtandaoni hadi ngazi ya kaya.
Katika hatua nyingine, ripoti hiyo imetambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari vilivyoshiriki katika kampeni hiyo. Miongoni mwao ni Bongo FM kupitia kipindi cha Power Bank, ambacho kiliendesha mijadala ya kina kuhusu usalama wa watoto mitandaoni kwa kushirikisha wataalamu na wazazi moja kwa moja hewani. Pia, blogu maarufu ya Fullshangwe imetajwa kwa mchango wake mkubwa katika kuandika na kusambaza makala mbalimbali kuhusu kampeni hiyo tangu ilipozinduliwa Februari 2024.
Mbali na hivyo, redio za kijamii, runinga, na magazeti yamechangia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha jamii, huku namba ya msaada ya mtoto (116) ikiripotiwa kushuhudia ongezeko la simu kutoka kwa watoto na wazazi waliopata elimu kupitia vyombo hivyo.
Kamati ya COP imetoa wito kwa Wizara ya Elimu kuangalia uwezekano wa kuingiza elimu ya usalama wa mtandao katika mitaala rasmi ya shule za msingi na sekondari, ili kuimarisha mafanikio haya kwa kizazi kijacho.
Wadau mbalimbali wamesisitiza kuwa mafanikio haya ya mashuleni yanapaswa kuendelezwa kwa kuweka utaratibu wa kufundisha stadi za kidijitali kama sehemu ya mtaala, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa shule na wazazi katika malezi ya kidijitali.
“Kwa sasa, shule zimekuwa ngome ya kwanza ya ulinzi wa mtoto katika ulimwengu wa teknolojia. Hii ni hatua muhimu kwa taifa letu,” imesema taarifa ya kamati hiyo.