Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa hakutakuwa na nafasi ya kuongeza muda wa utekelezaji wa Mradi wa Huduma ya Maji kwa Miji 28, huku Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb), akitoa onyo kali kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo.
Akizungumza jijini Dodoma katika kikao na wakandarasi na washauri wa mradi huo, Waziri Aweso ameeleza kuwa makubaliano ya mkataba ni lazima yaheshimiwe.
“Sitakubali kuona mkandarasi yeyote anakuja na hoja ya kuongeza muda. Hakutakuwa na majadiliano ya muda wa nyongeza. Tunataka kazi ikamilike kwa wakati kama tulivyokubaliana,” Waziri Aweso amesisitiza.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 60 katika baadhi ya maeneo, lakini bado kuna changamoto ya kasi ndogo katika maeneo mengine.
Aweso amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Oktoba 2025, huduma ya maji imeanza kutolewa katika miji yote inayohusika,
“Huu si mpango wa kawaida tu; ni wajibu wa kitaifa. Wakandarasi na washauri lazima wachukue jukumu hili kwa uzito unaostahili,” Aweso amesema.
Ametaja miji inayopaswa kuwa imekamilika kufikia Septemba/Oktoba 2025 kuwa ni pamoja na Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa Masoko, Manyoni, Geita, huku miji mingine kama Ifakara, Njombe, Makambako, Sikonge, Kasulu, na Mpanda ikitarajiwa kukamilika Desemba 2025.
Waziri Aweso pia ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi na msaada wake, Serikali ya India kwa ushirikiano wao, pamoja na jamii na mamlaka za mikoa kwa uvumilivu wao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote ili kuhakikisha mradi huo haukwami kwa namna yoyote ile.
Aidha, amesema changamoto zote zinazojitokeza lazima zifike mapema Wizarani ili hatua stahiki zichukuliwe haraka, kwa dhumuni la kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati na kwa ufanisi.
Mradi wa Huduma ya Maji kwa Miji 28 unalenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 5 mijini na asilimia 3 vijijini, na tayari unatekelezwa katika miji mbalimbali nchini, ukitarajiwa kuwanufaisha zaidi ya Watanzania milioni 6.9.
Mradi huo una thamani ya shilingi trilioni 1.58 za Kitanzania, ambapo miji 24 inatekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya India kwa gharama ya Sh. trilioni 1.167, na miji mingine minne ikifadhiliwa kwa fedha za ndani zenye thamani y bilioni 413.