SERIKALI imeendelea kuchukua hatua thabiti katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuanzisha sera mpya, kuleta mageuzi ya sheria, na kutoa vivutio vya kiuchumi vinavyowezesha ukuaji wa uwekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Akizungumza katika jongamano la wawekezaji la Tanzania na India liliofanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 15, 2025, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (Mb), ameeleza kuwa serikali kupitia taasisi mbalimbali imeweka mikakati madhubuti ya kurahisisha mchakato mzima wa biashara na uwekezaji nchini.
Pia Kigahe alibainisha kuwa serikali imeanzisha Sera ya Maendeleo Maalum ya Uchumi (Special Economic Development Policy – SEDP) na Sheria Na. 6 ya mwaka 2020, inayoripoti moja kwa moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sheria hiyo inalenga kuimarisha usimamizi, uratibu na uendelezaji wa maeneo maalum ya kiuchumi na kuchochea utekelezaji wa bajeti ya maendeleo.
Katika mageuzi hayo, serikali imeanzisha Kituo Kimoja cha Kimataifa cha Uwekezaji (World Trade Center) kinachojumuisha zaidi ya taasisi 14 zinazoshughulika na utoaji wa leseni, vibali, vyeti na huduma za ufadhili wa uwekezaji.
“Kwa sasa, muda wa kushughulikia maombi ya leseni na vyeti vya uwekezajiumepunguzwa kutoka siku 14 hadi 7 tu za kazi, sambamba na mfumo wa utatuzi wa migogoro ya uwekezaji katika ngazi ya kimataifa.” Amesema
Tanzania pia ni mwanachama wa mikataba muhimu ya kulinda wawekezaji, ikiwemo: Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA), African Trade Insurance Agency (ATI), International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID).
Akizungumzia Vivutio vya Kodi kwa Wawekezaji Kigahe amesema kuwa Kupitia Tume ya Uwekezaji Tanzania (TIC), serikali inatoa vivutio vya kiuchumi vikiwemo:
Msamaha wa Kodi ya Mapato kwa hadi miaka 10, Msamaha wa Withholding Tax kwenye riba na gawio, Msamaha wa kodi kwenye malighafi na bidhaa adimu, Upunguzaji wa Corporate Tax, na urahisi wa upatikanaji wa ardhi kwa miradi ya kimkakati.
Kigahe amebainisha sababu kuu zinazowafanya wawekezaji kutoka India na mataifa mengine kuichagua Tanzania kuwa ni uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya Tanzania na India unaoendelea kwa zaidi ya miaka 50.
Pia Amani na utulivu wa kisiasa, inayoiweka Tanzania katika nafasi ya juu barani Afrika na sera rafiki za biashara, zinazojali sekta binafsi na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kupitia TIC.
Serikali pia inajivunia kuwa na idadi kubwa ya vijana wenye nguvu kazi, vipaji na elimu, pamoja na raslimali za viwanda katika sekta kama Kilimo, Uvuvi na Ufugaji wa Samaki, miundombinu, madini, nishati, vifaa tiba na dawa, TEHAMA na Mawasiliano na huduma za Kifedha.
Licha ya hayo Naibu Waziri Kigahe amehimiza wawekezaji kutoka India na mataifa mengine kuchangamkia fursa lukuki zinazopatikana nchini Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hili limejiandaa kuwa kitovu cha biashara na viwanda vya Afrika Mashariki na Kati.
Kwa upande wa Balozi wa Tanzania Nchini India, Anisa Mbega amesisitiza kuwa ziara hii ni ushahidi wa dhamira ya pamoja ya Tanzania na India kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali.
“India inaongoza duniani katika sekta za dawa, kilimo, teknolojia ya afya na uchakataji wa mazao. Sekta hizi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Tanzania,” amesema
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka India hadi Tanzania umefikia thamani ya dola za Kimarekani bilioni 4.1 kati ya mwaka 1997 hadi Machi 2025, ukihusisha miradi 738 na kuleta ajira kwa zaidi ya watu 67,000. Sekta zilizofaidika ni pamoja na utalii, viwanda, usafirishaji, afya na kilimo.
Balozi Anisa amesema Tanzania inategemea kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za dawa na vifaa tiba kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka India.
“Kwa sasa, Tanzania inaagiza takribani asilimia 85 ya vifaa na dawa kutoka nje ya nchi, hali inayoweka fursa kubwa kwa uwekezaji katika sekta hiyo.”
Aidha, ushirikiano huu umeimarishwa zaidi kwa huduma ya moja kwa moja ya ndege kati ya Mumbai na Dar es Salaam kupitia Air Tanzania, ambayo hufanya safari nne kwa wiki. Huduma hii si tu hurahisisha biashara bali pia huimarisha uhusiano wa watu kwa watu.
Mwanzilishi, Marketing Assistance and Research Support (MARS), Rekha Sharma akizungumza katika jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na India amesema kampuni 30 kutoka India zimekuja kuangalia fursa za uwekezaji nchini Tanzania.
“Makampuni haya yanatoka katika sekta mbalimbali, ambapo makampuni 15 yanawakilisha sekta ya afya na tiba, sekta ambayo India ina uongozi mkubwa na kutambulika kimataifa.
Amesema Kupitia makubaliano ya ushirikiano baina ya MARS na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), taasisi zetu mbili zinashirikiana kwa karibu kukuza uwekezaji nchini Tanzania, hasa katika sekta za afya, kilimo, uzalishaji viwandani, na nishati mbadala.
Sekta ya Afya na Tiba, ni sehemu kubwa ya ujumbe wetu inajumuisha makampuni ya utengenezaji wa dawa, vifaa tiba, API (malighafi za dawa), na teknolojia za uchunguzi wa magonjwa.
Madawa ya Asili na Mitishamba, Kampuni moja inawakilisha bidhaa za mitishamba na tiba asilia za Ayurveda, ambapo India ni kinara duniani.
Dawa za Saratani, Kampuni maalum inayozalisha dawa za saratani kwa ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu ipo tayari kushirikiana na sekta ya afya ya Tanzania.
Vifaa vya Uchunguzi wa Magonjwa: Kampuni nyingine imeonyesha nia ya kuanzisha kiwanda nchini Tanzania kwa ajili ya utengenezaji wa vifaa vya uchunguzi wa magonjwa kama UKIMWI, saratani, na mengineyo.
Pia ameeleza kuwa kuna Mwekezaji mkubwa kutoka India ameonesha nia ya kuanzisha kiwanda cha kuchakata mafuta ya kupikia hapa nchini, ili kusaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje katika sekta hii.
Mbali na sekta ya afya, ujumbe huo pia unajumuisha makampuni kutoka sekta za Magari na vipuri, Magari ya umeme (e-vehicles), Vifaa vya kimatibabu na teknolojia ya reli.
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa Kongamano la Tanzania India.
Picha ya pamoja.