Ukurasa mpya wa Habari Afrika wazinduliwa na Rostam Azizi pamoja na Dkt. Mpango ambao unataka kuwepo kwa uwekezaji mkubwa katika vyombo vya Kidijitali na Ulinzi wa Taarifa Sahihi.
Amebainisha kuwa changamoto kubwa inayopo ni ongezeko la taarifa potofu na propaganda kupitia mitandao ya kijamii kunakodhoofisha imani ya wananchi kwa vyombo rasmi vya habari.
“Serikali ya Tanzania imeanza mchakato wa mageuzi ya sheria ya habari, ili iendane na katiba, viwango vya kimataifa vya haki za binadamu na matakwa ya zama za kidijitali. “amesema .
Kwa upande wake Rostam Azizi — Mmoja wa waanzilishi wa vyombo vikubwa binafsi vya habari nchini Tanzania — ameweka wazi umuhimu wa kuwekeza katika “miundombinu ya fikra” kwa ajili ya kujenga jamii inayojitambua, inayoheshimu ukweli na inayojenga simulizi zake kwa misingi ya kitaifa na kiafrika.
Kupitia Mjumbe wake Absalom Kibanda, Rostam alizungumzia historia ya uanzishaji wa vyombo kama Mwananchi Communications na New Habari Corporation, akibainisha kuwa vyombo vya habari si biashara tu, bali ni sehemu ya roho ya Taifa.
Aidha amesema kuwa , vyombo hivyo vinapaswa kuwa daraja la mawasiliano kati ya wananchi na mamlaka, na nguzo ya uwajibikaji na maendeleo.
“mitandao mingi ya kimataifa leo imekuwa chanzo cha taarifa zisizo sahihi kuhusu Tanzania na Afrika kwa ujumla — taarifa ambazo haziangalii maslahi ya wananchi wa bara hili, haziheshimu mila na hazitoi uwajibikaji wowote kwa jamii zinazolengwa”amesema .
Hata hivyo amesema suluhisho si kudhibiti uhuru wa habari, bali ni kuwekeza katika majukwaa ya ndani ya kuzalisha na kusambaza habari zenye mizizi ya kitaifa, kwa kutumia teknolojia za kisasa, vijana wabunifu, na waandishi waliobobea katika taaluma.
“Tanzania haiwezi kuongoza katika maendeleo ya uchumi bila kuongoza pia katika ujenzi wa mifumo ya habari yenye weledi. Alisema kuwa ni wakati wa kuwekeza katika uzalishaji wa taarifa sahihi kama tunavyowekeza kwenye barabara, viwanda na huduma nyingine za msingi, kwa kuwa taarifa ni miundombinu ya fikra na dira ya Taifa “amesema.
Aidha hotuba hizi mbili zimepokelewa kwa heshima kubwa na washiriki wa kongamano hilo kutoka nchi mbalimbali za Afrika, wakiwemo viongozi wa mabaraza ya habari, wahariri wakuu, watunga sera, wanazuoni na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.