Madereva wa mabasi yanayofanya safari zake kuanzia Stendi kuu ya mabasi Mbeya wamehimizwa kufuata na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
Akizungumza na madereva hao Julai 17, 2025 Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoani humo linaendelea na oparesheni mbalimbali za ukamataji wa makosa ya usalama barabarani ikiwemo makosa hatarishi.
“Mbali na ukamataji tunaoendelea kufanya, leo tupo hapa Stendi Kuu ya Mabasi Mbeya kwa lengo la kutoa elimu na kuwakumbusha madereva kutii sheria za usalama barabarani, kuepuka kufanya makosa hatarishi na kuzidisha abiria ili kuepuka ajali na madhara yake” alisema SSP Kilewa.
Naye, Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mhandisi Rajabu Ghuliku amewataka madereva kuheshimu haki za abiria kwa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora ya usafirishaji bila kuwepo kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria.
Akizungumza kwa niaba ya madereva wengine, Dereva wa kampuni ya Superfeo Express Prosper Kilongo amesema kuwa kitu cha msingi kwa madereva ni kufuata sheria kwani mabasi mengi yamefungwa VTS hivyo dereva kwenda mwendo kasi ni maamuzi yake binafsi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa magari kabla ya kuanza safari pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na abiria ili kuwajengea uelewa na kuwakumbusha wajibu wao wawapo barabarani kwa lengo la kuzuia na kudhibiti makosa ya usalama barabarani.