Na Mwandishi wetu, Kiteto
MWENGE wa uhuru mwaka 2025 umeridhia na kuikubali miradi yote sita ya maendeleo iliyoipitia ambayo ina thamani ya shilingi 1,412,757,592.5 .
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025, Ismail Ussi ameipongeza Kiteto kwa miradi bora ya maendeleo, hamasa na mwamko waliyokuwa nayo wakazi wa eneo hilo.
“Nawapongeza DC Kiteto mtu bingwa kabisa Mheshimiwa Remidius Mwema, Mheshimiwa Mbunge Edward Ole Lekaita, kaka lao na dada lao DED wetu CPA Hawa Hassan Abdul na mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan mama lao,” amesema Ussi.
DC Kiteto Mhe Remidius Mwema ametaja miradi sita iliyopitiwa na mwenge ni uzinduzi wa jengo jipya la zahanati ya Ngabolo ambapo mwanamke mjamzito alijifungua mtoto wa kiume na kuridhia kumpa jina la Ismail la kiongozi wa wakimbizi mwenge kwani alizaliwa wakati mwenge ulipofika Ngabolo.
Mwema amesema mwenge wa uhuru umetembelea mradi wa kikundi cha vijana Weredi studio na pia kuzindua mradi wa ujenzi wa daraja la barabara ya Kibaya Mbeli.
“Pia mwenge wa uhuru umezindua mradi wa ujenzi wa shule ya msingi ya mkondo mmoja ya Oloimugi, kutembelea uboreshaji miundombinu na usambazaji wa maji Kibaya mjini na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa ghala la kuhifadhi mazao,” amesema Mwema
Mbunge wa Jimbo la Kiteto wakili msomi Mheshimiwa Edward Ole Lekaita Kisau, amewashukuru na kuwapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kujitokeza kwa wingi kuulaki mwenye wa uhuru.
Ole Lekaita amesema mwenye wa uhuru ukiwa Kiteto umetembelea, kukagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo yote ni kwa ajili ya ustawi na manufaa ya wananchi wa Kiteto.
“Naishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha nyingi na kufanikisha miradi hii ya maendeleo iliyopitiwa na mwenge wa uhuru, ambayo wananchi wa Kiteto wanatamba nayo,,” amesema Ole Lekaita.
Mmoja kati ya wakazi wa Kiteto, Kulwa Mkamba amesema mwenge wa uhuru umekuja na neema katika eneo hilo kwani pamoja na kufungua miradi ya maendeleo pia jamii imenufaika kiuchumi.
“Madereva wa bodaboda wamenufaika, baba lishe na mama lishe wameuza vyakula, vinywaji na nyumba za kulala wageni nazo zimetumika kutoa huduma,”amesema Mkamba.