Mwamvua Mwinyi, Pwani
Julai 19, 2025
MKOA wa Pwani unatarajia kugawa vyandarua 971,939 katika kampeni ya ugawaji wa vyandarua bure kwa kaya 426,637, kampeni itakayoanza Agosti 15, 2025.
Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini ifikapo mwaka 2030.
Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Menejimenti , Serikali za Mitaa, Utawala na Fedha, George Nsajigwa, alisema hayo wakati akizindua kampeni ya uhamasishaji na ugawaji vyandarua mkoani Pwani kwa niaba ya Katibu Tawala mkoani humo katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Nsajigwa alieleza kuwa kampeni hiyo itatekelezwa katika kata 108 na vijiji/mitaa 426, ambapo kaya 426,637 zenye jumla ya watu takribani milioni 1,633,774 watanufaika.
“Kampeni hii inalenga kutokomeza malaria nchini, na inaratibiwa kwa pamoja na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), pamoja na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI,” aliongeza Nsajigwa.
Kwa mujibu wa Nsajigwa, mkoa wa Pwani umepiga hatua katika mapambano dhidi ya malaria, ambapo kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 15.3 mwaka 2016 hadi asilimia 6.7 mwaka 2022.
Hata hivyo, hali ya maambukizi inaendelea kupungua mwaka 20222 ilikuwa asilimia 20 hadi kufikia 2025 imefikia asilimia 15.
Aidha, idadi ya vifo vitokanavyo na malaria imeshuka kwa asilimia 27 kutoka vifo 110 hadi 30, hatua ambayo Nsajigwa alisema imechangiwa na matumizi sahihi ya vyandarua kwa makundi maalum kama watoto, wajawazito na wazee, pamoja na unyunyiziaji wa dawa za kuua viluwiluwi vya mbu na usafi wa mazingira.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, alieleza mkoa umeanza kampeni ya uhamasishaji kuanzia ngazi ya wilaya, kwa lengo la kuondoa kabisa ugonjwa huo.
Alibainisha kuwa mkoa umepokea lita 24,000 za dawa ya kuua viluwiluwi wa mbu, kwa ajili ya kuondoa mazalia ya mbu katika mazingira.
Peter Gitanya, kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), alisema ugawaji wa vyandarua unapaswa kwenda sambamba na uhamasishaji wa matumizi yake kwa jamii ili kufanikisha mapambano dhidi ya malaria.
Alisisitiza , Serikali imeweka mkakati madhubuti kuhakikisha kila kaya inapokea vyandarua bora vya kujikinga na mbu waenezao malaria.
Akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe – Dkt. Rashid Mfaume, Stella Kanyange kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, alifafanua Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inajivunia mafanikio makubwa katika kupunguza ugonjwa wa malaria.
“Nchini tupo asilimia 8.1 , tumepunguza ugonjwa huo wa maralia kwa asilimia 15 mwaka 2017 ambapo kwa mwaka 2022 imeshuka kwa asilimia 45 na kufikia asilimia 8.1;” alieleza Stella.
Alielezea mapambano hayo, yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima na kuhimiza “Mimi, wewe, na Tanzania bila malaria kufikia 2030 – inawezekana.”