Na Fauzia Mussa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimesisitiza dhamira yao ya kulinda faragha na taarifa binafsi za wananchi, huku zikitambua mchango mkubwa wa maofisa na waandishi wa habari katika kufanikisha jukumu hilo nyeti katika zama za kidigitali
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa maofisa habari wa taasisi za serikali na wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), yaliyofanyika katika ukumbi wa BOT, Kinazini, Mjini Unguja.
“Ulinzi wa taarifa binafsi ni msingi wa utu na haki za binadamu. Dunia inashuhudia ongezeko la taarifa zinazovuja kupitia mitandao na vyombo vya habari, hali inayohatarisha heshima na usalama wa watu. Nawasihi waandishi na maofisa habari kuwa makini na kazi zao, kuhakikisha hawavunji faragha za watu kwa kisingizio cha habari,” alisisitiza Dk. Khalid.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ni muhimu sana kwa kuwa yatawajengea uwezo washiriki kuhusu namna bora ya kuchuja taarifa nyeti, hasa katika kipindi nyeti cha kuelekea uchaguzi mkuu, ambacho mara nyingi huambatana na upotoshaji na uvunjifu wa faragha.
“Hatupaswi kutumia teknolojia kuchafua utu wa watu kwa kisingizio cha uhuru wa habari. Nawasihi kujenga utamaduni wa kuandika habari zenye kulinda heshima za watu,” alisema Dk. Khalid.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa PDPC Zanzibar, Rehema Khaimis Abdalla, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wadau hao kuhusu wajibu wao katika kulinda taarifa binafsi za wananchi, kwa kuwa wao ndio wakusanyaji na wasambazaji wakuu wa habari.
“Katika zama hizi za kidigitali, taarifa husambaa kwa kasi kubwa. Waandishi wa habari wanapaswa kufahamu uzito wa jukumu lao katika kulinda taarifa binafsi, sambamba na kutoa habari sahihi na kwa wakati,” alisema Rehema.
Akitoa mada, Innocent Mungy alifafanua kuwa taarifa binafsi ni zile zinazoweza kumtambulisha mtu moja kwa moja kama hali ya afya, mahusiano, hali ya kifedha, au anuwani, na kwamba wamiliki wa taarifa hizo wana haki ya kuzilinda dhidi ya watu wasiotakiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Emmanuel Mkilia, alieleza kuwa katika kipindi hiki cha kukua kwa teknolojia, uvujishaji wa taarifa binafsi unaweza kusababisha madhara makubwa kama vile wizi wa fedha, unyanyapaa na hata kusababisha migogoro ya kijamii.
“Faragha ni utu wa mtu. Kazi ya waandishi ni kutoa taarifa sahihi bila kuvunja sheria, na siyo kuwakejeli au kuwavunjia heshima watu. Tunahitaji maadili katika taaluma hii ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa,” alisisitiza Dk. Mkilia.
Mafunzo hayo yamepokelewa vyema na wanahabari washiriki ambao wamesema yatawawezesha kubadili namna wanavyoripoti habari na kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki na faragha katika kazi zao za kila siku