Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22,2025 jijini Dodoma kuhusu kufunguliwa rasmi kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi waliohitimu Kidato cha Sita mwaka 2025 na waliokidhi vigezo vya kupata ufadhili wa masomo ya sayansi kupitia mpango wa Samia Scholarship.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22,2025 jijini Dodoma kuhusu kufunguliwa rasmi kwa dirisha la maombi ya ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi waliohitimu Kidato cha Sita mwaka 2025 na waliokidhi vigezo vya kupata ufadhili wa masomo ya sayansi kupitia mpango wa Samia Scholarship.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakaonufaika na ufadhili wa Samia Scholarship kwa mwaka 2025 kutoka wanafunzi 650 hadi kufikia 1,051, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya wanafunzi 400 kutoka mwaka uliopita.
Akizungumza leo Julai 22, 2025, Jijini Dodoma na waandishi wa habari , Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema ongezeko hilo linatokana na bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu.
Ufadhili huo, ambao unalenga kuwasaidia wanafunzi waliopata matokeo bora katika masomo ya sayansi, umetajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukuza taaluma za kisayansi kwa vijana wa Kitanzania.
“Wakati tunaanza tulikuwa na uwezo wa kuwafadhili wanafunzi 650 kwa mpigo mmoja. Kwa mwaka huu, bajeti imeturuhusu kufikia wanafunzi 1,051, na kati yao wanafunzi 51 ni wale wenye mahitaji maalum waliopata daraja la kwanza.”.”amesema Prof. Mkenda
Ufadhili huo unalenga maeneo ya kipaumbele ya TEHAMA, Hisabati, Elimu Tiba, Sayansi na Uhandisi.
Aidha, kati yao wanafunzi 50 watafadhiliwa masomo nje ya nchi katika maeneo ya Akili Unde (Artificial Intelligence), sayansi ya Data na masomo yanayohusiana na fani hizo ambao pia watapaswa kuomba kupitia mpango maalum wa Samia Extended Scholarship AI/DS/AI+.
Amebainisha kuwa majina ya Wanafunzi wenye vigezo yanapatikana katika tovuti ya Wizara na ile ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Waziri Mkenda pia amebainisha kuwa wanafunzi watakaomba ufadhili wa Samia Skolashipu Extended DS / AI + watapitia mafunzo ya miezi kumi katika kambi maalum ya maarifa ( Boot Camp) itakayofanyika katika Taasisi ya Nelson Mandela ili kuwaandaa vyema kujiunga na programu hizo pamoja na masuala mengine muhimu ikiwemo uzalendo.
Mpango wa Samia Scholarship umeendelea kuwa chachu ya kuwainua vijana kitaaluma na kuwajengea uwezo katika sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa kulingana na Dira ya Taifa 2050.
Katika hatua nyingine amezungumzia kuhusu kufutwa kwa baadhi ya kozi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof.Mkenda amesema idadi ya wanafunzi watakaokwenda kusoma chuo hicho ipo pale pale na kozi zilizofutwa zina mabadiliko katika kuleta umahiri kwenye masomo ya kufundishia ya sayansi na Sanaa kutokana na awali ilijikita kufundisha namna na kufundisha.