Na Fauzia Mussa
Zanzibar imeeleza dhamira yake thabiti ya kukuza Uchumi wa Buluu kwa kuwekeza kwa vijana na wanawake, kushirikiana na wadau wa kikanda, na kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Mwadini Juma Hatibu, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia, alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu, Kepteni Hamad Bakar Hamad, katika ufunguzi wa Mkutano wa Kikanda wa Wadau wa Sekta ya Bahari uliofanyika kwenye ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano wa TradeMark Africa, Sekretarieti ya AfCFTA na Mastercard Foundation, Mhandisi Hatibu alisema kuwa Zanzibar inalenga kujenga uchumi wa baharini ulio jumuishi, unaostahimili mabadiliko ya tabianchi na wenye kuleta maendeleo kwa wananchi, hususan wavuvi wadogo, wanawake na vijana.
> “Uchumi wa Buluu ni msingi wa maendeleo ya Zanzibar. Tunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na jamii ili kufungua fursa za ajira, lishe bora na utunzaji wa mazingira ya bahari,” alisisitiza.
Alitaja maeneo ya kipaumbele ya Zanzibar kuwa ni pamoja na uvuvi, ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, utalii wa baharini, usafirishaji na biashara ya baharini, nishati mbadala, bioteknolojia na matumizi endelevu ya rasilimali za majini.
Hata hivyo, alitaja changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo ikiwemo miundombinu duni, ukosefu wa mitaji kwa wajasiriamali, udhaifu wa sheria na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akasema kuwa Zanzibar imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha miundombinu ya uvuvi, kuongeza upatikanaji wa masoko na mitaji kwa vijana na wanawake, na kuwekeza katika tafiti na teknolojia ili kufanikisha utekelezaji wa sera za kikanda kama AfCFTA na EAC.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Sekretarieti ya Ziwa Victoria – EAC, Sindi Kasambala, alieleza kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha uwezo wa kiuchumi kwa wanawake na vijana kupitia mnyororo wa thamani wa bidhaa za uvuvi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
> “Wanawake na vijana ni mhimili wa sekta ya uvuvi, lakini wamekuwa wakikosa fursa za masoko na mitaji. Tunahitaji sera rafiki, elimu ya biashara, na miundombinu bora ili kufanikisha ushiriki wao katika uchumi wa buluu,” alisema Kasambala.
Washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Kenya, Uganda, Nigeria, Zambia, DRC, Comoros, Tanzania bara na visiwani, walielezea matumaini kuwa mkutano huo utaleta suluhisho la changamoto zinazowakabili, kama ukosefu wa vifaa, elimu ya uchakataji wa bidhaa, ubaguzi wa kijinsia, na miundombinu duni ya uhifadhi.
Mkutano huo wa siku tatu unatarajiwa kuhitimishwa kwa kutoa maazimio ya pamoja kuhusu usimamizi wa rasilimali za baharini, upatikanaji wa masoko, na mbinu za kuvutia uwekezaji katika sekta ya Uchumi wa Buluu kote Afrika – kwa kuangazia nafasi ya wanawake na vijana kama injini kuu ya mageuzi hayo.