Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja,alipotembelea shule ya Sekondari Masonya Wilayani humo jana.
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja amesema,mradi wa skimu ya umwagiliaji unaotekelezwa katika kijiji cha Nambalapi kata ya Masonya Wilayani humo kwa gharama ya Sh.bilioni 60.3 utakamilika kwa muda uliopangwa.
Masanja amesema hayo jana,alipokuwa akizungumza na wakazi wa kiijiji cha Nambalapi wakati wa ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi Wilayani Tunduru.
“Nawahakikishia wananchi kuwa,mradi huu ambao ni wa kimkakati utakamilika kama ulivyopangwa kwani ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya yetu na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla,nawaomba sana muwe wavumilivu na kumpa mkandarasi ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake”alisema Masanja.
Amewataka wananchi,kutunza na kulinda miundombinu ya mradi huo ambao unatarajiwa kuchochea uchumi wa Wilaya ya Tunduru na Mkoa wa Ruvuma kwa wananchi hususani wakulima kulima majira yote ya mwaka badala ya kutegemea mvua za masika.
“Miundombinu hii yote inapaswa kulindwa kikamilifu na nyinyi wananchi ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija inayokusudiwa,mradi huu wa skimu ya umwagiliaji ni muhimu sana kwenu nyinyi na Serikali kwa ujumla”alisema Masanja.
Amewahimiza wakulima,wapanue ukubwa wa mashamba na kuongeza uzalishaji ili kujikwamua na umaskini kwani katika Wilaya ya Tunduru,bado kuna ardhi kubwa inayofaa kwa mazao mchanganyiko, badala ya kutegemea zao moja la korosho.
Aidha Masanja,amepiga marufuku wakulima kuuza mazao kwa njia ya kangomba kwa kutumia vipimo haramu ambavyo vinachangia kuwanyonya na kuwarudisha nyuma kiuchumi, badala yake wahakikishe wanauza kwenye vyama vyao vya ushirika.
Amewataka viongozi wa vyama vya ushirika,kuhakikisha wanatenda haki kwa kutowaibia wakulima wanapofikisha mazao yao kwenye maghala na kuwalipa fedha kwa wakati ili kutoigombanisha Serikali na wananchi wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Marando alisema,mradi wa skimu ya umwagiliaji Nambalapi unalenga kukuza uzalishaji kwa njia endelevu na bora zaidi.
Alisema,jumla ya hekta 300 zitatumika na wanufaika ni wakulima zaidi 4,000 wa vijiji vya Sisi kwa Sisi,Temeke,Mkalikamwana,Masonya,Nambalapi,Chingurunguru na Tunduru Mjini.
Mwakilishi wa mkandarasi kampuni ya Africentiric Company Ltd inayojenga mradi huo Yusuph Luvanda alisema,lengo la mradi ni kuboresha maisha ya wakulima kwa kuwapatia miundombinu bora ya umwagiliaji,kuongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo kupitia sekta ya kilimo.
Luvanda,ametaja kazi zinazotekelezwa ni uchimbaji na maandalizi ya msingi wa kibanio cha maji,ujenzi wa muundo wa kudumu wa zege,kufunga vifaa vya kudhibiti mtiririko wa maji na kuunganisha banio la maji na mfereji mkuu kwa ajili ya kusambaza maji mashambani na kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa katika mardi huo.