Na WAF – Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuchukua uamuzi wa kuhamia katika Mji wa Serikali Mtumba na kuzitaka Wizara ziingine kuiga mfano huo.
Waziri Lukuvi ametoa pongezi hizo leo Julai 23, 2025 alipofanya ziara ya kutembelea jengo jipya la Wizara ya Afya lililopo katika mji wa Serikali Mtumba, baada ya Wizara hiyo kuhamia rasmi na kutoa huduma katika jengo hilo kuanzia Julai 21 2025.
“Nimekuja kwa lengo la kukagua na kuangalia hali ya maendeleo ya majengo yetu, ambao bado hawajamaliza tuweze kuwasukuma ili nia njema ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ionekane, ametoa pesa zote kwa lengo la kuona majengo yanakamilika na watumishi wote wanahamia kwenye mji wa Serikali,” amefafanua Waziri Lukuvi.
Aidha, Waziri Lukuvi amewaagiza wajenzi wa majengo ya mji wa Serikali Mtumba pamoja na wasimamizi wa majengo hayo ya Wizara kukamilisha kwa haraka ili Wizara zote zihamie na kufanya kazi kwa pamoja.
“Hii itarahisisha sana kwa wananchi wanaotoka mikoani kuja kwa shughuli mbalimbali, kutembelea Wizara hii na wakifika hapa wanaweza kuzipata wizara zote kwa mara moja na kero zao zote zikahudumiwa katika eneo moja,” amesema Waziri Lukuvi
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe awali akimkaribisha Waziri Lukuvi amesema, watumishi wote wa Wizara ya Afya wamehamia katika mji wa Serikali Mtumba isipokuwa kwa taasisi chache ambazo zinalazimika kubaki zilipo kutokana na umuhimu wa kuendelea kuwepo katika maeneo husika.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi na Majengo wa Wizara ya Afya Bw. Johnson Kamala amesema ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 96 hadi sasa na jengo hilo linatarajia kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo mwezi Agosti mwaka huu, ambalo litakuwa limegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 26.6.