Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Msumbiji amekutana na Mhe. Dkt. Victor Matemandada, Balozi wa Jamhuri ya Zimbabwe nchini Msumbiji. Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kwa Mhe. Balozi Hamad kujitambulisha na pia kujadiliana na Mhe. Balozi Matemadanda masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili leo Julia 24, 2025.
Mhe. Balozi Matemadanda alieleza kuridhishwa na uhusiano wa nchi yake na Tanzania na kusisitiza haja ya uhusiano huo kuimarishwa. Aidha, alisisitiza haja ya Mabalozi wa Nchi za Afrika waliopo Msumbiji, hususan kutoka nchi za Jumuiya ya SADC, kufanya kazi kwa ukaribu ili kufanikisha malengo ya Jumuiya hiyo na kwa maslahi mapana ya nchi zote wanachama.
Katika kuimarisha uhusiano wa Kikanda, Mhe. Balozi Matemadanda alihimiza nchi za SADC kufanya biashara zaidi baina yao tafauti na ilivyo sasa ambapo nchi nyingi za Kiafrika ikiwemo za SADC hupendelea kufanya biashara na nchi zilizoendelea.
Vilevile, aliipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maandalizi mazuri ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, 2025. Aliiombea Tanzania kukamilisha uchaguzi huo utakaohusisha ngazi ya; Urais, Wabunge/Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani, kwa salama na amani.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Hamad alimshukuru Mhe. Balozi Matemadanda kwa kukubali kukutana nae na ukarimu aliopatiwa. Aidha, alieleza kuridhishwa na uhusiano wa muda mrefu na kidungu baina ya Tanzania na Zimbabwe, tokea wakati wa harakati za Ukombozi na kutoa rai ya uhusiano huo kuimarishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
Mhe. Hamad pia alishauri kuhusu haja kwa Nchi za Kusini mwa Afrika na zilizojirani na Msumbiji, kuisaidia nchi hiyo katika mapambano dhidi ya ugaidi yanayoendelea Kaskazini mwa nchi hiyo kwa kuwa vitendo hivyo visipodhibitiwa, vitasambaa katika nchi na maeneo mengine ya jirani.
Vilevile, Mhe. Balozi Hamad alielezea jitihada zinazofanywa na Ubalozi wa Tanzania – Maputo katika kutangaza Lugha ya Kiswahili sambamba na mipango ya karibuni ya kufungua Kituo cha Utamaduni ambacho pamoja na mambo mengine, kitatumika kufundishia Lugha ya Kiswahili na kutangaza Utamaduni wa Kitanzania.