Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametumia ziara yake nchini Belarus kunadi fursa za uwekezaji katika maeneo manne ya kipaumbele ya Serikali ya awamu ya sita ambayo ni kilimo, afya, madini na ulinzi & usalama.
Mhe. Waziri Mkuu katika siku mbili za ziara yake, tarehe 22 na 23 Julai 2025 ametembelea kampuni kubwa nane zenye nguvu ya mitaji jijini Minsk na kuzihakikishia utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana nazo kwa kuzipatia kila aina ya msaada zitakapokuja Tanzania kuwekeza.
Kwenye eneo la kilimo, Mhe. Waziri Mkuu alikutana na viongozi wa kampuni ya AFTRADE ambayo tayari ipo nchini na kuwasisitiza kuongeza kasi katika kuendeleza kilimo hususan kuwa na programu za kuwasaidia wakulima wadogo mitaji, utafiti na mafunzo ili kilimo kiweze kuwa na tija, kizalishe ajira na kuongeza usalama wa chakula nchini.
Katika eneo hilo la kilimo, Waziri mkuu pia alitembelea chuo cha kilimo cha Belarus na viwanda vya matrekta na kuvishawishi viwanda hivyo kufungua matawi nchini Tanzania.
Kuhusu chuo cha kilimo ambacho mafunzo yake huyafanya kwa vitendo zaidi, Waziri Mkuu aliomba Watanzania wapatiwe fursa za masomo katika chuo hicho ili waweze kuendeleza sekta ya kilimo nchini, watakapomaliza masomo yao.
Kuhusu Afya, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kampuni ya kuzalisha na kusambaza dawa na vifaa tiba ya Belmedepreparaty ambayo ni moja ya kampuni kubwa nchini Belarus. Kampuni hiyo inayozalisha bidhaa tofauti tofauti zaidi ya 1700 na kuuza ndani na nje ya nchi katika mataifa zaidi ya 24, iliridhia maombi ya Mhe. Waziri Mkuu na kuahidi kufanya ziara nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.
Mhe. Waziri Mkuu alisema Belmedepreparaty ni kampuni sahihi kuja kuwekeza nchini kutokana na kutumia teknolojia ya kisasa ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.
Kwa upande wa sekta ya madini, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo inayotumika kuchimba madini migodini na kukishawishi kiwanda hicho kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Kuhusu suala la Ulinzi na Usalama, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ukoaji na kuzima moto na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na kiwanda hicho ili kuondoa tatizo la uhaba wa vifaa hivyo nchini.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake na aliondoka Julai 24, 2025 kurejea nyumbani.