DIBAJI
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kama mnavyofahamu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhakikisha kuwa kazi inaendelea kwa kudumisha tunu za Taifa letu, kukuza uchumi wa nchi, na kuimarisha ustawi wa wananchi. Amekuwa akifanya hivi kupitia miongozo na maelekezo anayotoa kwa viongozi na watendaji wa Serikali kwenye shughuli mbalimbali.
Aidha, amekuwa akitoa nasaha na rai kwa Watanzania kushirikiana, kushikimana na kuwa kitu kimoja katika kulijenga Taifa.
Vilevile, Rais Dkt. Samia anayeongoza Serikali sikivu amekuwa anakutana yeye mwenyewe na wananchi, wadau na makundi mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kuhakikisha hoja walizonazo zinapatiwa ufumbuzi na kuimarisha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi.
Ni kutokana na hayo ninayo furaha kubwa sana ya kuwaletea jarida hili la Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu linaloelezea shughuli mbalimbali ambazo zinafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kupitia jarida hili linalotoka kila mwezi utaona namna ambavyo maono na uongozi wa Rais Dkt. Samia yanavyogusa kila nyanja ya maisha ya Mtanzania.
Vilevile kupitia kazi anazozifanya kwa ushirikiano na Viongozi wenzake na wananchi utaona sio tu msisitizo wake wa kazi kwa maendeleo, bali pia namna Rais Dkt. Samia anavyoishi ahadi yake kuwa “kazi hii sitoifanya peke yangu bali nitashirikiana na Watanzania wote”.
Ninawatakia usomaji mwema
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu