*UKukamilika kwa daraja hilo kutanufaisha Kata tano
Iramba – Singida
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la zege katika Mto Kinkungu lenye urefu wa mita 65.6 linalojengwa katika barabara ya Mtoa-Ndago Kata ya Shelui Wilayani Iramba kutanufaisha wananchi wa Kata tano Wilayani humo.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Kamati ya Ukaguzi ya TARURA ikihitimisha Ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani Singida.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahim Kibasa ameileza Kamati hiyo kuwa Mradi wa ujenzi wa daraja hilo unalenga kuboresha mawasiliano kati ya Kata za Shelui, Mtoa, Ndago, Mtekente na Urughu na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli za maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii katika Kata hizo.
“Licha ya changamoto zilizojitokeza katika hatua za utekelezaji, mradi umefikia hatua ya kuridhisha na matarajio ni kuwa utakamilika ndani ya muda uliopangwa ambao ni Septemba 15, 2025” alisema
Akielezea hali ilivyokuwa hapo awali Mzee Ali Hassan Jumanne ambaye ni Mkazi wa Shelui amesema kuwa hali ilikuwa mbaya, watu walikuwa wanahatarisha maisha yao kuvuka mto Kinkungu hasa kipindi cha masika ambapo maji hujaa katika Mto huo na wale waliokuwa wakijaribu kuvuka walisombwa na maji.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutujengea daraja hili, tunamshukuru Rais Mama Samia kwani huko nyuma tuliahidiwa kujengewa daraja hili na haikuwa hivyo lakini alipoingia madarakani Mama Samia amefanya ndoto zetu kuwa za kweli, tunamshukuru sana Mama”.
Akitoa taarifa ya majumuisho ya ziara yao ya Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA CPA. Ally Rashid amesema kuwa kimsingi miradi yote waliyoitembelea kwa ujumla wake hatua iliyofikia sio mbaya ni hatua nzuri isipokuwa inahitajika kuendelea na usimamizi na kuhakikisha yale mapungufu machache ambayo wameyainisha yanafanyiwa kazi katika hatua hiyo ya mwisho ya ukamilishaji wa miradi hiyo.
Katika taarifa hiyo pia amesisitiza suala la uzingatiaji wa ubora katika utekelezaji wa miradi na sio kukimbizana na muda tu hususani kwenye Miradi ya dharura sambamba na utekelezaji wa miradi hiyo iendane na thamani ya fedha zilizotumika.