Na Meleka Kulwa – Dodoma
CHUO cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kimeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari nchini kuhusu uandishi sahihi wa taarifa za Mahakamani.
Mafunzo hayo yamefanyika Julai 25, 2025 kwa njia ya mtandao, yakiwahusisha zaidi ya waandishi wa habari 150 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yameelezwa kuwa sehemu ya kuimarisha uandishi makini wa habari za Mahakamani na kuwahakikishia wananchi kupata taarifa sahihi na zenye ukweli.
akizungumza na waandishi wa Habari, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema kuwa taarifa zinazohusu Mahakama ni nyeti, hivyo zinahitaji uangalifu mkubwa katika namna zinavyoandikwa.
Amesema kuwa hata makosa madogo kama ya matumizi ya alama za uandishi (punctuation marks) yanaweza kusababisha taharuki kwa mtu anayehusika na hata kwa jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa wakufunzi wa mafunzo hayo ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mwanahabari, Alloyce Komba, aliyebainisha maeneo muhimu ambayo waandishi wa habari wanapaswa kuyazingatia wanapochakata habari za Mahakamani.
Amesema kuwa ni muhimu kwa mwandishi wa habari kufahamu muundo wa Mahakama nchini, ikiwa ni pamoja na majukumu ya kila ngazi ya Mahakama, majina rasmi ya Mahakama hizo pamoja na vyeo sahihi vya Majaji, Mahakimu na waendesha mashtaka.
“Wengi wetu tumezoea kuandika Mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu, lakini usahihi wake ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, ingawa tumeizoea kuitambua kwa jina la Kisutu kutokana na eneo ilipo,” amesema Wakili Komba.
Ametaja pia vyanzo halali vya habari za Mahakamani kuwa ni ndani ya Mahakama zenyewe, kutoka kwa Majaji, Mahakimu, Makarani, Mawakili, waendesha mashtaka pamoja na washtakiwa wenyewe.
Aidha, amewahimiza waandishi wa habari kuacha kuweka maoni yao binafsi kuhusu mwenendo wa kesi, na badala yake wajikite kuripoti kile tu kilichojiri Mahakamani.
Kwa upande wake, Afisa Habari, Elimu na Mawasiliano Mwandamizi wa Mahakama ambaye pia ni mwanasheria, Faustine Kapama, ameonya juu ya mambo yasiyopaswa kuripotiwa ikiwa ni pamoja na kutaja majina au kuonyesha picha za watoto, mashahidi na waathirika katika kesi zinazohusiana na udhalilishaji