TIMU ya Fountain Gate FC imemtambulisha mchezaji chipukizi Juma Issa Abushiri (Chuga) kutoka timu ya taifa ya vijana ya Tanzania (U-17). Nyota huyo amesaini mkataba wa miaka mitano kuwa kwenye timu hiyo ambayo ina uhakika wa kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ya NBC ambayo ni namba nne kwa ubora msimu wa 2025/26.
Akizungumza katika Hoteli ya Tanga Beach Resort jijini Tanga, baada ya kumsainisha mchezaji huyo, Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau, amesema kuwa usajili huo ni sehemu ya kuendeleza utamaduni wa timu hiyo wa kuwapa nafasi vijana.
Ameeleza kuwa Juma Issa ni zao la timu za vijana za Fountain Gate tangu akiwa mdogo, na alisoma katika shule za timu hiyo, ambako kipaji chake kiligunduliwa.
Amesema kuwa lengo la kuwasajili vijana ni kuwapa fursa ya kuonesha ushindani katika Ligi Kuu na kufungua milango ya kucheza soka nje ya nchi.
Aidha, katika msimu uliopita, timu hiyo ilipandisha vijana takriban wanane walio chini ya umri wa miaka 20, ambao wamepata nafasi ya kuonesha uwezo wao katika timu ya wakubwa.
Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Mbuzi ameweka wazi kuwa mpango mkubwa wa timu hiyo ni kufanya vizuri kwa msimu mpya na timu ambazo ziliwafunga hazitawafunga msimu mpya wa 2025/26.