Kiungo nyota wa kimataifa kutoka Zambia, Clatous Chama, amesema kuwa klabu ya Simba SC inapendwa na kuheshimiwa zaidi nchini kwao Zambia ikilinganishwa na Yanga SC.
Chama ambaye ameachana na Yanga, amesema kuwa staili ya mpira ya klabu ya Simba, historia yake barani Afrika, pamoja na uwepo wake wa mara kwa mara kwenye michuano ya kimataifa, kumeifanya ipate umaarufu mkubwa miongoni mwa wapenzi wa soka nchini Zambia.
“Simba ni timu kubwa sana na inapendwa mno Zambia. Ukija Zambia, mashabiki wengi wanaifuatilia Simba na wanajua hata wachezaji wake kwa majina. Yanga si kwamba haijulikani, ila haijafikia levo ya Simba kwa kupendwa Zambia,” alisema Chama.
Kauli hiyo imeibua mijadala mitandaoni, hasa kwa mashabiki wa Yanga ambao wameonekana kupinga vikali kauli hiyo wakisema kuwa timu yao kwa sasa ina ushawishi mkubwa Afrika Mashariki na Kati, na imeanza kujenga jina hata kimataifa.