DAR ES SALAAM: KIUNGO mkabaji wa kimataifa kutoka Uganda, Khalid Aucho, hatimaye ametangaza rasmi kuhitimisha ukurasa wake ndani ya klabu ya Yanga baada ya kuitumikia kwa mafanikio katika misimu minne mfululizo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Aucho aliwashukuru viongozi, benchi la ufundi, wachezaji wenzake na mashabiki wa Yanga kwa kumbukumbu zisizosahaulika, huku akitaja kipindi chake ndani ya klabu hiyo kama “sura isiyoweza kusahaulika katika maisha yangu”.
“Katika misimu minne iliyopita, nimepata hisia kali. Tulifikia malengo ya ajabu na kujenga kumbukumbu zisizofutika. Tulishinda mataji ya ligi, tukasherehekea kila ushindi kama familia, na kushinda vizuizi kwa uamuzi na ujasiri,” aliandika Aucho.
Uamuzi wa kuagana na Yanga unafungua milango kwa kiungo huyo mwenye uzoefu kujiunga na timu nyingine. Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa klabu ya Singida Black Stars imeonesha nia ya dhati ya kumsajili kiungo huyo haraka iwezekanavyo.
Aucho ameondoka akiwa ni sehemu muhimu ya mafanikio ya Yanga, akihusika katika ushindi wa mataji mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya ndani, huku pia akiisaidia timu kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/23.
Wakati mashabiki wa Yanga wakimtakia kila la heri, macho sasa yanahamia Singida kuona kama watafanikiwa kumsajili nyota huyo haraka kama wanavyotamani.
The post Aucho aipa ‘Thank you’ Yanga first appeared on SpotiLEO.