LONDON: Tume huru ya Udhibiti wa wachezaji ya shirikisho la soka la England (FA) imemfutia Kiungo wa kati wa West Ham Lucas Paqueta mashtaka ya kuharibu mchezo na kupanga matokeo takriban miaka miwili baada ya Chama cha Soka nchini humo kuanzisha uchunguzi dhidi yake.
FA ilianza uchunguzi Agosti mwaka 2023 na mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil alishtakiwa rasmi mwezi Mei mwaka jana kwa madai ya kujitafutia kadi nyekundu kimakusudi kwa madhumuni maovu ya kuathiri michezo ya kubashiri kosa ambalo angefungiwa maisha kama angepatikana na hatia.
Mashtaka manne dhidi yake yalihusiana na mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Leicester City Novemba 12, 2022, pamoja na mechi za 2023 dhidi ya Aston Villa iliyopigwa Machi 12, Leeds United iliyopigwa Mei 21 na Bournemouth Agosti 12. Tume ya udhibiti ilibaini mashtaka haya manne kuwa “hayajathibitishwa” baada ya kusikilizwa.
Paqueta pia alishtakiwa kwa makosa mawili ya kushindwa kutoa ushirikian kwenye uchunguzi baada ya kukiuka Kanuni ya FA F3 kuhusu madai ya kushindwa kufuata sheria ya FA Kanuni F2, ambayo inahusiana na kutoa taarifa na nyaraka kwa wachunguzi.
Winga guyo alikanusha mashtaka haya pia lakini tume hiyo ya udhibiti iligundua kuwa yamethibitishwa na itaamua adhabu inayofaa kwa ukiukaji huu haraka iwezekanavyo.
The post Kisa ‘kubeti’ Paqueta anusurika kufungiwa maisha first appeared on SpotiLEO.