DAR ES SALAAM: KIUNGO mshambuliaji, Morice Abraham amejiunga na kikosi cha Simba akitokea klabu ya Spartak Subotica ya Serbia kwa mkataba wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa mtandao wa Simba, Baada ya kurejea nchini kutoka Serbia, Morice (21) alifanya mazoezi na timu ambapo kocha Fadlu Davids na wasaidizi wake walimpitisha hivyo Uongozi ukamsajili moja kwa moja.
Morice ambaye amekulia katika Kituo cha kukuzia vipaji cha Alliance Academy cha jijini Mwanza anakumbukwa kuwa na nahodha wa timu ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kilichoshiriki AFCON mwaka 2019 ambayo Tanzania ilikuwa mwenyeji.
Uwajibakaji na kujituma kwakwe uwanjani ni moja ya sifa iliyolivutia benchi la ufundi kutokana na kuonekana ana uchu wa mafanikio na yupo tayari kusaidia timu wakati wowote.
Msimu uliopita akiwa katika klabu yake ya Spartak Subotica, Morice amefunga mabao mawili na kusaidia kupatikana kwa mengine manne.
Morice atajiunga na kikosi kilichopo kambini nchini Misri muda wowote kutoka sasa mara baada ya kukamilika kwa vibali vyake vya kusafiria.
The post Morice Abraham ni mnyama first appeared on SpotiLEO.