Za ndani ndani kutoka Yanga wamedai kwamba Sowah hana nidhamu. Sio kwa sababu alikunjana na wachezaji wa Yanga katika pambano la fainali za Shirikisho pale Unguja, hapana, wanadai wamefuatilia mienendo yake katika timu yake kwa muda mrefu. Kuanzia Singida yenyewe na timu alizopita.
Kwa sababu ni Mghana hatuwezi kushangaa sana. Mkononi tuna kesi ya Mghana mwingine anayeitwa Bernard Morrison. Alikuja hapa nchini kimya kimya lakini ghafla akaanza kuwasumbua wakubwa. Kipaji chake na maisha yake vilikuwa vitu tofauti.
Baadaye kabisa maisha yake ya nje ya uwanja yaliwaelemea wakubwa. Kipaji walikiona na walikitamani lakini mwishowe wakatema bungo. Nataka kuamini kwamba Yanga waliamua kutema bungo mapema kwa Sowah lakini Simba wamekubali kulimeza. Kuna kitu wamekiona.
Tangu waachane na Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu hawajawahi kuwa na mshambuliaji wa maana pale mbele. Wamepita wengi. Alipita hata Papaa Jobe. Wakaja kina Leonel Ateba. Mashabiki na wanachama hawajawahi kuridhika. Mabosi pia nao wanajua kwamba wamejidanganya
Kwa Sowah, hakuna shabiki au mwanachama ambaye ataulaumu uongozi kama akifeli. Wamemuona Sowah akifika nchini na wanajua ambacho amefanya. Tatizo ni kama kamari yao italipa kwa Sowah. Sio kuhusu mabao, bali kuhusu maisha yake binafsi ndani na nje ya uwanja
Simba imeamua kuchukua mabao yake. Naweza kuwaelewa Simba kwa sababu wanahitaji mabao yake kuliko kitu kingine chochote kile kwa sasa. Mara nyingi nimekuwa nikisema hapa kwamba dunia imekumbwa na uhaba wa washambuliaji. Sio Afrika tu wala Tanzania.
Simba wameamua kwamba bora uwe na Sowah mwenye matatizo ya nidhamu kuliko Ateba asiye na matatizo ya nidhamu. Hata mimi ningekuwa kiongozi wa Simba ningechukua msimamo huo. Tunawajua washambuliaji wengi waliokuwa na vichwa vya moto lakini klabu ziliamua kuishi nao
Kwa upande wa Yanga pia kuna kesi ya kujibu kwa Injinia Hersi. Vipi mambo yakiwa kimya upande wa pili na Sowah akaendelea kuibuka shujaa huku Boyeli akifeli. Kutakuwa na maswali mengi dhidi yake kuhusu uamuzi wake wa kuachana na mtu ambaye walimuona kwa macho yao pale Singida kisha wakaenda kwa mtu ambaye hawakumuona kabla.
— Legend, Edo Kumwembe. [Mwanaspoti]