LOS ANGELES: Mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur Son Heung-min amekiri kuhamia Los Angeles FC inayoshiriki ligi kuu ya Marekani (MLS) halikuwa chaguo lake la kwanza lakini mazungumzo na rais wa klabu hiyo yalibadilisha moyo wake na kujiunga na klabu hiyo kwa ada iliyoweka rekodi MLS.
Kituo cha televisheni cha BBC Sport kimefahamu kuwa LAFC imelipa ada ya zaidi ya Euro milioni 20 kwa nahodha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili wenye chaguo la nyongeza ya miaka mingine miwili zaidi.
Son alifichua katika mkutano na wanahabari Jumamosi kuwa ataondoka Tottenham baada ya miaka 10 katika klabu hiyo. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alishuhudia ushindi wa LAFC wa 2-1 wa Kombe la Ligi dhidi ya Tigres UANL ya Mexico City juzi Jumanne.
Imeelezwa kuwa Ada ya usajili iliyolipwa kwa Spurs kwa Mkorea huyo inapita rekodi ya awali ya MLS ya Euro milioni 16.5 iliyolipwa na Atlanta United kumsajili Emmanuel Latte Lath kutoka Middlesbrough mwezi Februari.
“Ndoto imetimia. Kusema ukweli, halikuwa chaguo langu la kwanza. Lakini simu ya kwanza niliyopigiwa na John Thorrington) (rais mwenza wa LAFC) baada ya msimu wangu kumalizika ilibadilisha mawazo yangu alifanikiwa kubadilisha moyo na ubongo wangu alinionesha mahala sahihi zaidi pa kuwa. Sasa niko hapa na nimefurahi.” – amesema Son
Son anajiunga na timu ya LAFC ambayo kwa sasa ni ya sita kwenye kanda ya Magharibi (Western Conference) na anaungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Tottenham mlinda lango Hugo Lloris. Alicheza mechi yake ya mwisho Tottenham katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu mpya Spurs ikitoa sare ya 1-1 dhidi ya Newcastle mjini Seoul Korea Kusini.
Baada ya kuwasili kutoka Bayer Leverkusen mwaka 2015 alifunga mabao 173 katika mechi 454 alizoichezea Spurs. Alikuwa nahodha wakati Tottenham ilipoifunga Manchester United katika fainali ya Europa League mwezi Mei na kutwaa taji lao la kwanza baada ya miaka 17.
The post “LAFC haikuwa chaguo langu” – Son first appeared on SpotiLEO.