LONDON, Mabingwa wa Europa League Tottenham Hotspur wametangaza kuwa kiungo wa kati wa klabu hiyo James Maddison atakosekana kwa kipindi cha makisio kisichozidi miezi saba baada ya madaktari wa klabu hiyo kusema kuwa atafanyiwa upasuaji baada ya kuumia mshipa wa goti.
Maddison alipata jeraha hilo wakati wa mechi ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Newcastle United Jumapili iliyopita na alitolewa nje kwa machela baada ya kushindwa kuendelea na mchezo huo.
Meneja wa Spurs Thomas Frank alisema baada ya mchezo huo kuwa ni goti lile lile la mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aliloumia mwezi Mei ambalo lilimlazimu Maddison kukaa nje katika mechi za mwisho za msimu uliopita.
“Tunaweza kuthibitisha kwamba James Maddison atafanyiwa upasuaji wa kupasuka kwa Anterior Cruciate Ligament (ACL) katika goti lake la kulia,” sehemu ya taarifa ya klabu hiyo ilisema.
Mchezaji huyo alifunga mabao 12 na kutoa asisti 11 katika mashindano yote msimu uliopita Spurs ikishinda taji la Europa na kumaliza ukame wa miaka 17 wa kutwaa mataji. Tottenham hawakutoa ratiba rasmi ya kurejea kwake lakini majeraha ya ACL huwa yanawaweka nje wachezaji kwa kipindi cha angalau miezi sita kabla ya kuanza mazoezi tena.
Spurs wataanza msimu wao kwa mtanange wa UEFA Super Cup dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Paris St Germain mjini Udine, Italia tarehe 13 Agosti kabla ya kuanza kampeni ya Ligi kuu ya England wakiwa nyumbani dhidi ya Burnley siku tatu baadaye.
The post Maddison nje miezi saba first appeared on SpotiLEO.