Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) leo limefanya droo ya hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) na Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) na droo hiyo imefanyika kwenye studio za Azam TV ikihusisha timu kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, zikiwemo sita kutoka Tanzania.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), Tanzania Bara inawakilishwa na Simba SC na Yanga SC huku Zanzibar ikiwakilishwa na Mlandege SC ambapo Simba imepangwa kucheza na Gaborone United ya Botswana ambayo itaanza ugenini, Yanga watakutana na Wiliete Benguela ya Angola vilevile kuanzia ugenini huku Mlandege wao wakivaana na Ethiopian Insurance ya Ethiopia. Timu hizi tatu zinatarajiwa kuwakilisha nchi kwa ushindani mkubwa.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), wawakilishi ni Azam FC, Singida Black Stars kutoka bara na KMKM kutoka Zanzibar, Azam FC itakutana na El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini, Singida Black Stars watacheza na Rayon Sports ya Rwanda huku KMKM wakipangwa dhidi ya AS Port ya Djibouti.