Nguli wa soka duniani, Cristiano Ronaldo (40), hatimaye amemvisha pete ya uchumba mpenzi wake wa muda mrefu, Georgina Rodríguez, pete kubwa na ya kifahari inayofaa hadhi ya bilionea.
Georgina alionyesha pete hiyo mpya kupitia ukurasa wake wa Instagram, ikithibitisha rasmi uchumba wao, huku mashabiki wakivutiwa na muonekano wa kifahari wa pete yenye jiwe kuu la oval likiwa limepambwa na mawe mawili madogo pembeni.
Ingawa wawili hao hawajathibitisha mtengenezaji wa pete hiyo, wataalamu wamekadiria thamani yake kuwa kati ya dola milioni 2 hadi 5 (sawa na takribani shilingi bilioni 5 hadi 12 za Kitanzania).
Kwa mujibu wa Ajay Anand, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Rare Carat, jiwe hilo kuu huenda ni la rangi ya kiwango cha juu (D color) na ubora wa juu kabisa (flawless clarity), lenye uzito unaoweza kuzidi carats 30 — hali inayoweza kufanya thamani yake kufikia hadi $5 milioni.