Ifahamu Gaborone United Wapinzani wa Simba Ligi ya Mabingwa CAF 2025/2026
Wababe wa kulisakata kabumbu wa Tanzania Bara na Visiwani Simba SC, Yanga SC, Azam FC, Singida Black Stars, KMKM na Mlandege SC wameshajua wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kwa hatua ya awali ya kufuzu makundi. Droo hiyo, iliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, ilishuhudiwa na magwiji wa soka wa zamani, akiwemo Sunday Manara aliyeichezea Yanga na Abdallah Kibadeni aliewahi ichezea Simba, wote wakikumbukwa kwa mchango wao mkubwa miaka ya 1970.
Katika matokeo ya droo hiyo iliyohusisha michuano ya ligi ya mabingwa Afrika na ile ya kombe la shirikisho, mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wamepangwa kuvaana na Wiliete Benguela ya Angola, huku Simba SC wakipangwa kuanza kampeni zao dhidi ya Gaborone United kutoka Botswana, na Mlandege SC wakikutana na Insurance ya Ethiopia.
Historia Fupi ya Gaborone United
Gaborone United ni moja ya klabu kongwe zaidi nchini Botswana, ikiwa na historia ndefu iliyoanza mwaka 1967 takribani miaka 58 iliyopita. Ni timu yenye heshima kubwa kwenye soka la ndani, ikiweka alama kupitia mafanikio mbalimbali kwenye mashindano ya kitaifa.
Msimu uliopita wa Ligi Kuu Botswana, Gaborone United walimaliza kileleni wakiwa na pointi 66, wakifunga jumla ya mabao 56 na kuruhusu 23 pekee, huku wakipoteza mechi nne pekee msimu mzima. Mafanikio yao yametokana na uimara wa kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji wa ndani na wachache kutoka Kenya, Namibia, Zambia na Afrika Kusini.
Mataji na Mafanikio
Gaborone United imewahi kutwaa mataji kadhaa nchini, yakiwemo:
- Ligi Kuu ya Botswana
- FA Challenge Cup
- Mascom Top 8 Cup
na mashindano mengine ya ndani. Hata hivyo, historia yao kwenye michuano ya kimataifa haijawahi kufikia hatua ya makundi.
Rekodi ya Kimataifa
Klabu hii imeshiriki michuano ya CAF mara tano bila mafanikio makubwa.
- Ushiriki wa kwanza ulikuwa 1987 kwenye African Cup of Champions Clubs na tena mwaka 1991, lakini safari zote zilikomea hatua za awali.
- Mwaka 2010, walicheza Ligi ya Mabingwa na kufika raundi ya pili, kisha kuangukia Kombe la Shirikisho ambapo pia walitolewa mapema.
- Mwaka 2022/23, baada ya kutwaa ubingwa wa ligi, walishiriki tena Ligi ya Mabingwa lakini safari yao ikaishia kwenye hatua ya awali.
Mbinu na Mfumo wa Uchezaji
Kocha wa sasa wa Gaborone United ni Dimitar Pantev, raia wa Bulgaria, ambaye hupendelea zaidi kutumia mfumo wa 4-2-3-1 na mara nyingine 4-3-3. Mfumo huu unalenga uwiano kati ya kushambulia na kulinda, ukitumia wachezaji wa pembeni kuongeza kasi na nafasi za mashambulizi. Hii inawafanya wawe na mtindo usio mbali sana na ule unaotumiwa na kocha wa Simba SC, Fadlu Davids.
Wachezaji Muhimu wa Kutazama
- Thatayaone Kgamanyane – Mshambuliaji mwenye kasi na uwezo wa kuingia katikati, alimaliza msimu uliopita akiwa mfungaji wa pili bora wa ligi na mabao 14 kwenye mechi 26.
- Mpho Kgaswane – Kiungo wa ulinzi mwenye ubunifu, pasi za hatari, na uwezo wa kupiga mashuti ya mbali.
- Molaodi Tlhalefang – Kiungo mkabaji anayeweza kutuliza mchezo na kuisogeza timu mbele.
Udhaifu wa Kikosi
Licha ya uimara wao wa ndani, Gaborone United ina changamoto kadhaa:
- Wanapokutana na timu zenye mashambulizi makali kama Simba SC, hucheza kwa kujilinda sana (“kupaki basi”), jambo ambalo mara nyingi huwagharimu.
- Wanaathirika wanapocheza mbele ya mashabiki wengi, kwani presha huwafanya kushindwa kutekeleza mpango wao wa mchezo ipasavyo.
- Wachezaji wao wengi hawana uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa zenye ushindani mkubwa.