DAR ES SALAAM: MKESHA wa muziki wa taarabu utakaohusisha mastaa na wakongwe wa muziki huo nchini utarajiwa kufanyika Agosti 28, mwaka huu katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.
Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Kampuni ya Chocolate Princess Limited waandaaji wa tamasha hilo, Mboni Masimba amesema tamasha hilo ni bure na limeandaliwa mahsusi kwa wadau wa Chama cha Mapinduzi CCM, likibeba kauli mbiu “Wanamwambao tunatamba na Mama”.
Amesema limepangwa karibu na kampeni kwasababu limelenga kutoa hamasa kwa wapenzi wa muziki huo kushiriki pamoja kwa burudani lakini pia, kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hili ni tamasha la kishua lenye ladha ya taarabu ya kipekee. Tutaanza saa 10 jioni hadi majogoo, kisha kwa pamoja tutaelekea kwenye uzinduzi wa kampeni,” amesema Mboni.
Tamasha hilo linatarajiwa kuvuta mashabiki lukuki kutokana na orodha ndefu ya wakongwe wa taarabu akiwemo Khadija Kopa, East Afrika Melody, Sabah Muchacho, Khadija Yusuf, Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’, Mwanahawa Ally, Mzee Yusuf, Zanzibar One na Leila Rashid.
Kwa upande wake, Mzee Yusuf alisema taarabu ni muziki unaoibeba Tanzania kimataifa na kufafanua:
“Taarabu ni muziki wa kipekee. Ukienda dunia nzima, ukitaja taarabu watu wanaielekeza Tanzania. Muziki huu unaweza kuchezwa na rika zote bila kubagua. Tamasha hili limekuja kwa wakati muafaka.”
Palina Ninje, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania, amesema ameguswa kushiriki mkesha huo kwa kuwa unaleta sura mpya ya siasa na burudani.
“Siasa si mikutano pekee. Kupitia muziki wa taarabu, vijana wameajiriwa na vipaji vinajulikana. Tarehe 28 tutamsindikiza Rais Samia, kwa mara ya kwanza nchi yetu ikiingia kwenye historia kubwa ya kisiasa,” amesema Palina.
Aliwataka wanawake wote nchini, bila kujali vyama vyao, kujitokeza kumsapoti Rais Samia kupitia tamasha hilo na kwenye uzinduzi wa kampeni.
The post Mkesha wa Taarabu kufanyika Agosti 28 first appeared on SpotiLEO.