MOROGORO: KLABU ya Mtibwa Sugar imemtambulisha rasmi straika Datius Peter kama mchezaji wao mpya, ikimkaribisha katika familia ya “wakulima wa miwa” kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Akizungumza baada ya utambulisho huo, uongozi wa Mtibwa Sugar ulisema ujio wa Datius ni sehemu ya mpango wa kuimarisha safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha timu inakuwa na makali zaidi msimu ujao.
“Tunamkaribisha Datius Peter kwenye familia ya wakulima wa miwa. Ni mchezaji mwenye kipaji na ari ya ushindi, tunaamini atakuwa sehemu muhimu ya safu ya ushambuliaji na kuongeza chachu ya ushindani katika kikosi chetu,” ilieleza taarifa ya klabu.
Datius amejiunga na wakata miwa hao akitokea Kagera Sugar ambapo ameahidi kufanya kazi kwa bidii kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake.
“Nina furaha kubwa kuwa sehemu ya klabu hii yenye historia kubwa. Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kuisaidia Mtibwa Sugar kurejea kwenye nafasi ya juu kwenye ligi,” amesema.
Mtibwa Sugar, yenye maskani yake Turiani mkoani Morogoro, imerejea Ligi Kuu ikifanya usajili kwa lengo la kurejea kwenye ushindani mkali dhidi ya klabu kongwe za ligi, huku mashabiki wake wakisubiri kuona sura mpya ikiongeza uhai ndani ya kikosi.
Tayari kikosi hicho kimeanza kambi ya maandalizi Dar es Salaam kabla ya kurudi Morogoro kwa maandalizi ya mwisho ya Ligi Kuu.
The post Mtibwa Sugar yaanza na Datius Peter first appeared on SpotiLEO.