ROTTERDAM: MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Uholanzi Memphis Depay yuko fiti kuichezea timu hiyo katika mechi yao ya kufuzu Kombe la Dunia nyumbani dhidi ya Poland leo Alhamisi, mchezo ambao unaweza kumpa fursa ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa nchi hiyo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 aliifikia rekodi ya Robin van Persie ya mabao 50 katika mechi yao ya mwisho mwezi Juni wakati Waholanzi walipoishindilia Malta mabao 8-0 katika mechi ya pili katika Kundi G.
Kulikuwa na shaka juu ya utimamu wa Depay kwa mechi ya leo jijini Rotterdam lakini alirejea siku za karibuni katika klabu ya Corinthians nchini Brazil, na kocha Ronald Koeman aliwaambia waandishi wa habari jana Jumatano kwamba mshambuliaji huyo alikuwa fiti na yuko tayari kuanza mechi hiyo.
Depay, ambaye amecheza mechi 102, alifunga bao lake la kwanza la timu ya taifa kwenye Kombe la Dunia la 2014 dhidi ya Australia jijini Porto Alegre, Brazil, na kuwa mfungaji bora kijana zaidi wa Uholanzi wa michuano hiyo akiwa na umri wa miaka 20.
Katika harakati zao za kufuzu kwa fainali za mwaka ujao nchini Marekani, Canada na Mexico, Uholanzi wameshinda mechi zao mbili za kwanza za kufuzu michuano hiyo huku mchezo dhidi ya Poland ukiwa muhimu kwa nafasi yao ya kuongoza kundi hilo na kufuzu moja kwa moja.
The post Depay afukuzia rekodi Uholanzi first appeared on SpotiLEO.