SOFIA: TIMU ya taifa ya Hispania imeanza vyema kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia kwa ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Bulgaria katika mechi ya Kundi E usiku wa Alhamisi, mabao ya Mikel Oyarzabal, Marc Cucurella na Mikel Merino yote katika kipindi cha kwanza.
Oyarzabal aliipa Hispania mwanzo mzuri ndani ya dakika ya tano tu, akifunga bao lake la tano katika mechi zake sita za mwisho za kimataifa, baada ya Martin Zubimendi kumrahisishia kazi kwa asisti nzuri.
Lamine Yamal alionekana kuwa na uhakika wa kufunga bao lake, lakini kipa Svetoslav Vutsov alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kuokoa kwenye ‘near post’, kabla ya Hispania kupata bao la pili kwenye dakika ya 30 Cucurella akifunga bao lake la kwanza la timu ya taifa.
Dakika nane baadae kiungo mshambualiaji wa Arsenal Mikel Merino alipachika bao safi la ‘free header’ kutoka kwenye kona ya Lamine Yamal na kuwafanya Hispania kuwa mbele kwa mabao 3-0.
“Nadhani tulikuwa na kipindi cha kwanza kizuri sana, Timu iliwaka tangu mwanzo tulikuwa na nguvu, muunganiko mzuri, nafasi nyingi, na muda wote tulikuwa kwenye box la mpinzani.” meneja wa Hispania Luis de la Fuente aliwaambia wanahabari.
Kocha huyo baadae iliwatumia Rodri na Dani Carvajal, ambao wamerejea baada ya kupona majeraha ya ACL, na wote wawili wakicheza mechi yao ya kwanza ya kimataifa tangu ushindi wa 4-1 dhidi ya Uswizi takriban mwaka mmoja uliopita.
The post Hispania yafanya kweli kufuzu WC first appeared on SpotiLEO.