DAR ES SALAAM: WASANII wa muziki wa Bongo Fleva, Sharif Juma ‘Jay Melody’ na rapa wa kike Frida Amani, waliungana Agosti 18, 2025, kuachia wimbo wao mpya uitwao “Wewe na Mimi”, na matokeo ya ushirikiano huo yameanza kuonekana mapema.
Frida Amani, ambaye kabla ya kolabo hiyo alikuwa na wasikilizaji 722 pekee kwa mwezi kwenye jukwaa la Spotify, ameona ongezeko kubwa la usikilizwaji.
Tangu kuachiwa kwa wimbo huo, idadi ya wasikilizaji wake imepanda hadi kufikia 10,600 kufikia Septemba 5 zaidi ya wiki mbili tu tangu kuachiwa kwa wimbo huo.
“Wewe na Mimi” tayari imeanza kujipenyeza kwenye playlist mbalimbali za mashabiki na kushika nafasi kwenye chati za nyimbo zinazopendwa zaidi za Bongo Fleva kwenye majukwaa ya kidijitali.
Mbali na mafanikio ya namba, wimbo huu umekuwa ushahidi wa nguvu ya kolabo, ukionyesha jinsi ambavyo wasanii wanaweza kunufaika kwa kushirikiana, hasa kwa upande wa wasanii wanaochipukia.
Frida Amani sasa anaonekana kuvutia wasikilizaji wapya kwa kasi, jambo ambalo linampa nafasi ya kujijenga upya kwenye tasnia ya muziki.
Japokuwa Frida Amani bado yupo kwenye safari yake ya kujitambulisha zaidi kwenye muziki, ushirikiano wake na Jay Melody umeweka alama muhimu: nguvu ya pamoja inaweza kupeleka muziki mbali zaidi
The post Jay Melody, Frida Amani watisha Spotify first appeared on SpotiLEO.