NEWCASTLE: MCHEZAJI mpya wa Newcastle United Yoane Wissa atalazimika kusubiri kucheza mechi yake ya kwanza baada ya jeraha alilopata akiwa kwenye majukumu ya kimataifa kumfanya asiwe kwenye mpango wa mechi ya Jumamosi ya Ligi Kuu dhidi ya Wolverhampton Wanderers.
Wissa alisajiliwa kwa ada ya pauni milioni 55 kufuatia sakata la muda mrefu ya usajili ambapo klabu yake ya awali Brentford ilikataa mara kadhaa ofa kutoka Newcastle kwa ajili ya kumnunua fowadi huyo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alicheza mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia akiwa na jezi ya timu ya taifa ya DR Congo mwezi huu, akifunga dhidi ya Sudan Kusini na Senegal kabla ya kupata jeraha la goti.
Alipoulizwa kama atakuwa fiti kumenyana na Wolves katika mechi ya uwanja wa nyumbani, Howe aliwaambia waandishi wa habari: “Kwa bahati mbaya, hapana. Hatacheza mchezo huu, nilimuona kwa mara ya kwanza jana.
“Ana maumivu ya jeraha alilopata muda mfupi kabla hajatoka uwanjani. Kwa hiyo itabidi tuone maendeleo yake nadhani atakwenda kufanyiwa vipimo na labda amuone mtaalamu. Kwa bahati mbaya siwezi kukupa taarifa hiyo.”
Wissa, ambaye alifunga mabao 45 katika mechi 137 za Premier League akiwa na Brentford, na Nick Woltemade aliyesajiliwa kwa rekodi ya klabu watakuwa na jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji ya Newcastle, akiziba Pengo la Alexander Isak baada ya Msweden huyo kuhamia Liverpool.
The post Wissa bado bado Newcastle first appeared on SpotiLEO.