Kila msimu wa mpira wa miguu unapokaribia kuanza nchini Tanzania, macho na masikio ya mashabiki huzamia kwenye matamasha mawili makubwa Simba Day na Yanga Day (Siku ya Wananchi).
Matamasha haya yamekuwa zaidi ya hafla za michezo, yamegeuka kuwa majukwaa ya burudani, biashara na ubunifu huku kila klabu ikijitahidi kuonyesha ubora na kuwavutia mashabiki wake.
Simba Day 2025 iliyofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na kwa mara nyingine tena ilithibitisha heshima yake kama waanzilishi wa matamasha haya ya vilabu nchini.
Mashabiki walijitokeza kwa wingi mapema asubuhi, na kufurika uwanjani hadi tiketi zikaisha. Burudani kali kutoka kwa wasanii wakubwa wa Bongo Fleva huku Mbosso akiwa ndio mtumbuizaji mkuu na wote tumeshuhudia ile movie fupi aliyoionyesha ikionyesha ubunifu wa movie kama ya Mad Max, lakini ikatumika vyema na uigizaji uliovuta hisia, tunaweza kusema maandalizi yalikuwa ni makubwa sana kwenye kukamilisha movie ile, huku Mbosso akiandika kwenye ukurasa wake kama kuna muendelezo wa ile movie.
Mashabiki walipata pia nafasi ya kushuhudia utambulisho wa wachezaji wapya na jezi za msimu mpya zilipendezesha uwanja vilivyo. Hali ya ulinzi na usalama pia ilipewa kipaumbele, jambo lililoongeza hamasa na heshima ya tukio hilo.
Kwa upande mwingine, Yanga Day (Siku ya Wananchi) nayo haikubaki nyuma. Klabu hiyo ilitumia ubunifu kuandaa tamasha lililojaa burudani licha ya kwamba walikuwa na siku moja tu pekee ya kuhakikisha wanafanya maandalizi yao yote.
Katika upande wa burudani ulishikiliwa na Wasanii mbali mbali, huku Zuchu akiwa ndio msanii mkuu wa utoaji burudani, ambapo alikuja na ubunifu wake wa kipekee na pafomansi ya kimataifa ambayo tulizoea kuona wakina beyonce ndio wanafanya lakini tumeshuhudia hilo likifanyika Lupaso.
Kwenye mjadala wa ni tamasha lipi bora zaidi, ukweli ni kwamba matamasha haya mawili yanakamilishana kwa namna fulani. Simba Day ilionekana kushinda upande wa shangwe, idadi kubwa ya mashabiki na burudani kali, wakati Yanga Day ilibeba bendera ya ubunifu na maandalizi yenye mvuto ambayo yamefanyika kwa muda mfupi tu. Kwa ujumla, wote walitoa burudani ya kiwango cha juu na kuonyesha ukuaji wa soka nchini Tanzania.
Kwa mtazamo wangu, ikiwa tunazungumzia shangwe za mashabiki, Simba Day imependeza zaidi mwaka huu. Lakini kama kigezo ni ubunifu na maandalizi yenye taswira ya kimataifa, basi Yanga Day (Siku ya Wananchi) ndiyo imesimama kidete. Mwisho wa siku, matamasha haya mawili ni ushahidi kwamba soka la Tanzania limeendelea kukua na kuwaleta mashabiki pamoja katika kiwango cha juu zaidi.
Imeandikwa na George Chikao