NAIROBI:KLABU ya JKT Queens ya Tanzania imeandika historia ya kipekee baada ya kutwaa makombe yote makuu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kanda ya Cecafa 2025 yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Wanajeshi hao wa JKT Queens walitwaa Kombe la Ubingwa, huku pia wakinyakua tuzo za Nidhamu, Mchezaji Bora wa Mashindano Donisia Minja, Mfungaji Bora iliyoenda kwa Jamila Rajabu na Kipa Bora ni Najiath Abasi, jambo lililofanya Tanzania kung’ara zaidi kwenye soka la wanawake ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, JKT Queens iliwafunga Rayons Sports bao 1-0. Walionesha mchezo wa kuvutia na ushindani wa hali ya juu, wakihakikisha hawana mpinzani kwenye mashindano hayo.
Kwa mafanikio hayo, JKT Queens sio tu wamejihakikishia nafasi ya kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, bali pia wameipa heshima kubwa Tanzania.
Kocha Mkuu wa JKT Queens, Azishi Kondo, alisema alikuwa na uhakika timu yake ingetwaa taji hilo.
“Tulikuja hapa kwa lengo la kuchukua ubingwa na sasa dhamira hiyo imetimia. Nawashukuru wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya,” aliongeza Kondo.
Hii ni mara ya pili kwa JKT Queens kutwaa ubingwa wa kanda baada ya kulibeba taji hilo mwaka 2023. Sasa wao ndio timu pekee kushinda kombe hilo mara mbili, huku Vihiga Queens, Simba Queens na Commercial Bank of Ethiopia zikiwa zimetwaa mara moja kila moja.
The post JKT Queens yaondoka na makombe matano CECAFA first appeared on SpotiLEO.